Serikali ya Sudan: Watakaohalifu mpango wa kukusanya silaha watahukumiwa kifo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i44212-serikali_ya_sudan_watakaohalifu_mpango_wa_kukusanya_silaha_watahukumiwa_kifo
Makamu wa Rais wa Sudan Hassabu Mohamed Abdalrahman ameonya kuwa wapinzani wa mpango wa kukusanya silaha katika maeneo yenye mapigano na wale watakaohalifu kutekeleza mpango huo watashtakiwa na kuhukumiwa kifo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2018 12:25 UTC
  • Serikali ya Sudan: Watakaohalifu mpango wa kukusanya silaha watahukumiwa kifo

Makamu wa Rais wa Sudan Hassabu Mohamed Abdalrahman ameonya kuwa wapinzani wa mpango wa kukusanya silaha katika maeneo yenye mapigano na wale watakaohalifu kutekeleza mpango huo watashtakiwa na kuhukumiwa kifo.

Dakta Abdalrahman ametoa onyo kwa raia wa Sudan wasiotoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama vilivyopewa jukumu la kukusanya silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria katika maeneo yenye mapigano likiwemo la Darfur na kusisitiza kuwa adhabu ya kifo inawangojea wale wanaohalifu kutekeleza zoezi hilo.

Akihutubia semina ya mafunzo kwa viongozi wa bunge la jimbo la Darfur, Makamu wa Rais wa Sudan amesisitiza kuwa serikali haina mzaha na suala la kukusanya silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria na akaongeza kuwa hilo ni jambo la lazima kwa ajili ya kudumisha uthabiti nchini humo.

Siku chache zilizopita pia Hassabu Mohamed Abdalrahman aliashiria hasara za kiusalama, kijamii na kiuchumi zinazosababishwa na kuwepo silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria katika jamii na kueleza kwamba kuwepo kwa silaha hizo kumepelekea kuuawa watu wasio na hatia, raia kulazimika kuyahama makazi yao na kuvurugika amani na uthabiti kwa wakazi wa jimbo la Darfur.

Tangu mwaka mmoja nyuma serikali ya Sudan imeanza kutekeleza mpango wa kukusanya silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria katika maeneo yenye mivutano na machafuko yakiwemo ya Darfur na Kordofan Kusini kwa lengo la kurejesha amani na utulivu katika maeneo hayo.../