Kusimama kidete Wapalestina kwawalazimisha Wazayuni kuitisha kikao cha dharura
Viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamelazimika kuitisha kikao cha dharura baada ya vyama, mirengo na makundi yote ya Wapalestina kuungana na kusimama imara kukabiliana na uadui wa kupindukia wa rais wa Marekani dhidi ya mji mtakatifu wa Quds wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 6 Disemba 2017, Donald Trump alidharau sheria zote za kimataifa na hisia za walimwengu kwa kudai kwake kwamba eti Quds ni mji mkuu wa utawala pandikizi wa Israel. Wakati huo huo wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilitangaza kuwa tarehe 14 Mei 2018 itauhamishia Quds ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni.
Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limeripoti kuwa, kikao hicho cha dharura kimehudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa Israel kama mkuu wa jeshi la utawala huo wa Kizayuni, mkuu wa shirika la usalama wa ndani la Israel, Shabak, na mkaguzi mkuu wa polisi pamoja na maafisa waandamizi wa mashirika mengine ya usalama ya Israel.
Kilichowafanya viongozi hao wa ngazi za juu wa utawala wa Kizayuni kuitisha kikao hicho cha dharura ni wasiwasi wao kuhusiana na machafuko makubwa yanayoweza kutokea katikati ya mwezi huu wa Mei iwapo rais wa Marekani atatekeleza uamuzi wake wa kuuhamishia Quds ubalozi wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv.
Itakumbukwa kuwa tarehe 14 Mei 1948 ndiyo siku utawala wa Kizayuni ulipozipora rasmi ardhi za Wapalestina na kutangaza dola pandikizi la Israel. Tarehe hiyo ni maarufu kwa jina la Siku ya Nakama kati ya Wapalestina.