Tahadhari ya UN kuhusu mapigano zaidi CAR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i44260-tahadhari_ya_un_kuhusu_mapigano_zaidi_car
Ghasia zinazidi kupamba moto nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR jambo ambalo linamtia hofu kubwa Kamishna Mkuu wa haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
May 09, 2018 09:44 UTC
  • Tahadhari ya UN kuhusu mapigano zaidi CAR

Ghasia zinazidi kupamba moto nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR jambo ambalo linamtia hofu kubwa Kamishna Mkuu wa haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein

Kamishna huyo amenukuliwa leo kupitia taarifa ya ofisi yake akisema kuwa kinachomtia hofu zaidi ni kauli za chuki zinazotolewa kwa misingi ya dini pamoja na mauaji  ya hivi karibuni kwenye mji mkuu Bangui.

Amesema mauaji ya wiki iliyopita ya watu 22 yaliyotokea baada ya watu wenye silaha kuvamia kanisa yanadhihirisha ni kwa jinsi gani hali ni tete nchini CAR.

Bwana Zeid amesema vitendo hivyo vinachochea visasi kutoka jamii ya Wakristo akisema sasa mapigano yameenea na watu wanashambulia makazi, hospitali, makanisa na misikiti.

Amesema kwa kuwa uchochezi huo unafanyika pia kupitia mitandao ya kijamii, ana hofu kuwa mapigano kama ya wiki iliyopita yanaweza kuenea maeneo mengine kwa kasi kubwa.

Askari wa kulinda amani wa UN nchini CAR

Kamishna Zeid ametoa wito kwa pande husika kitaifa na kimataifa kuchukua hatua thabiti kuzuia mashabulizi kama hayo na ukiukwaji wa haki za binadamu. Amesisitiza kuwa ghasia za hivi karibuni katu zisiruhusiwe kuteketeza mchakato wa amani unaopigiwa shime na Muungano wa Afrika.

Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliibuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoka madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo, François Bozizé, huku mgogoro ukishadidi zaidi baada ya waasi wa Kikristo wenye kufurutu ada wa Anti-Balaka kuanzisha mauaji ya kutisha dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi. Hivi sasa kuna askari 10,000 wa kulinda amani katika nchi hiyo iliyo kati kati mwa bara la Afrika lakini hawajaweza kutuliza hali ya mambo na mapigano ya hapa na pale yangali yanaendelea.