May 15, 2018 14:14 UTC
  • Waislamu, Wakristo Uganda walalamikia kutozwa ushuru Misahafu, Biblia

Viongozi wa kidini nchini Uganda wamekosoa vikali hatua ya Mamlaka ya Kukusanya Ushuru nchini humo URA kuanza kutoza ushuru wa forodha suhula za kidini zinazoingizwa nchini humo kama nakala za Qurani na Biblia.

Ramadhan Mugalu, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu nchini Uganda amemtaka Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo kutekeleza ahadi aliyoitoa ya kutovitoza ushuru vitabu vya kidini vinavyoingia nchini humo.

Amesema, "Serikali imevuka mipaka sasa katika jitiada zake za kukusanya ushuru. Itawezekanaje kutoza kodi Neno la Mungu? Badala yake inapaswa kusaidia katika juhudi za kuchapishwa vitavu hivyo nchini."

Rais Museveni akiwahutubia Waislamu miaka ya huko nyuma

Naye Joshua Kitakule, Katibu Mkuu wa Baraza la Muungano wa Kidini nchini humo amesema, "Vitabu hivyo haviingizwi nchini kwa ajiili ya kupata faida, na hata iwapo serikali lazima itoze ushuru vitabu hivyo, hicho kiwango cha asilimia 18 ni cha juu mno."

Mkuu wa  Mamlaka ya Kukusanya Ushuru nchini Uganda URA, Doris Akol amesema serikali ilifanya makosa makubwa sana kuruhusu nakala za Qurani na Biblia, vitabu vya maombi na bidhaa nyingine za kidini kuingizwa nchini kwa miaka mingi bila kutozwa ushuru. 

Hivi karibuni serikali ya Uganda ilisema itaanza kutoza ushuru mitandao ya kijamii pia.

Tags