Apr 05, 2016 07:34 UTC
  • Machafuko yashtadi Brazaville, maelfu wakimbilia usalama wao

Maelfu ya wananchi wa Jamhuri ya Congo wameukimbia mji mkuu wa nchi hiyo Brazaville kutokana na kushika kasi makabiliano yaliyoripuka jana Jumatatu kati ya maafisa usalama na kundi moja la waasi.

Walioshuhudia wanasema mapigano hayo yalianza usiku wa kuamkia jana katika wilaya za Makelekele na Mayana baada ya kundi la waasi la Ninja kushambulia kambi za jeshi na vituo vya polisi. Aidha waasi hao wanadaiwa kuteketeza vituo vya umma mbali na kufunga barabara kuu za kuingia na kutoka mjini humo.

Thierry Moungalla, msemaji wa serikali ya Congo Brazaville amewalaumu waasi hao wa Ninja kutokana na machafuko haya mapya. Taharuki ingali imetanda nchini humo kutokana na milio ya risasi na mapigano hayo yanayoendelea katika baadhi ya maeneo ya Brazaville, ingawa hali imedhibitiwa kwa kiasi kikubwa na wanajeshi katika maeneo ya kusini ya mji mkuu. Mapigano baina ya serikali ya Congo na kundi la Ninja ambalo linataka kushirikishwa zaidi katika serikali yalianza miaka mingi iliyopita.

Kundi la Ninja lilikuwa miongoni mwa makundi ya upinzani katika vita vya ndani vya 1998 hadi 1999 na lilitia saini makubaliano ya amani na serikali mwaka 2003.

Mapigayo hayo yametokea wiki kadhaa baada ya Denis Sassou Nguesso kushinda tena kiti cha rais wa nchi hiyo kwa kupata asilimia 60 ya kura zilizopigwa.

Mapigano hayo yamezua wasiwasi kiasi kwamba Ufaransa, muitifaki mkubwa wa Congo Brazaville, imewatahadharisha raia wake walioko nchini humo na kuwataka wabakie majumbani mwao.

Tags