May 28, 2018 07:41 UTC
  • Uganda yakanusha taarifa kuhusu mlipuko wa Ebola nchini humo

Serikali ya Uganda imekanusha taarifa zilizoenea za kuibuka nchini humo ugonjwa hatari wa Ebola ambao umeua makumi ya watu katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokarasia ya Kongo.

Katika taarifa, Wizara ya Afya ya Uganda imekanusha habari kuhusu kuwepo kwa mlipuko wa homa ya Ebola nchini humo. Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya wa Uganda Bibi Sarah Opendi, inasema mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 35 alifariki Mei 21 kwenye eneo la Kakumiro, kutokana na homa ya Crimea-Kongo CCHF, na sio homa ya Ebola. Taarifa inasema wizara ya afya ya Uganda ina wasiwasi na ripoti kuhusu mlipuko wa Ebola kwenye eneo la Mubende nchini humo, na inataka kuujulisha umma kuwa hakuna maambukizi yoyote ya Ebola nchini humo.

Hayo yanajiri wakati ambao Wizara ya Afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo leo Jumatatu imeanza kutoa chanjo ya ugonjwa hatari wa Ebola katika vijiji viwili vilivyoathiriwa na mlipuko wa sasa wa maradhi hayo.

Mripuko wa hivi karibuni wa Ebola ndio wa tisa tangu ugonjwa huo uripotiwe huko DRC muongo wa 70. Kuripotiwa kesi za Ebola katika mji wa bandarini wa Mbandaka katika Mto Kongo kumeibua wasiwasi kuwa yamkini kirusi hicho hatari kikafika katika mji mkuu Kinshasa ambao una idadi ya watu milioni 10.

Chanjo ya Ebola

Shirika la Afya Duniani WHO limeonya kuwa mripuko wa Ebola nchini DRC umefikia kiwango hatari, na yumkini Ebola itaenea katika miji mingine huko DRC na hata nchi jirani iwapo ugonjwa huo hatari hautadhibitiwa. Shirika la Afya Duniani WHO limetaja nchi ambazo ziko hatarini kukumbwa na Ebola kuwa ni pamoja na Tanzania Angola, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Zambia.

Itakumbukwa kuwa, watu zaidi ya 11,000 walifariki dunia kutokana na mripuko wa ugonjwa  wa Ebola katika eneo la Afrika Magharibi mwaka 2014 hadi 2015, hususan kwenye nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia katika mripuko wa Ebola uliotajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani.

Tags