Wasimamizi wa uchaguzi Mali warefusha mgomo, uchaguzi mkuu matatani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46546-wasimamizi_wa_uchaguzi_mali_warefusha_mgomo_uchaguzi_mkuu_matatani
Wafanyakazi wa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi huu nchini Mali wametangaza kuwa wamerefusha mgomo wao, suala ambalo limezusha wasiwasi kuhusu zoezi hilo la kidemokrasia ambalo lilitazamiwa kuhitimisha miaka sita ya machafuko ya kisiasa na mashambulizi yanayofanywa na makundi yenye misimamo mikali.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 04, 2018 03:50 UTC
  • Wasimamizi wa uchaguzi Mali warefusha mgomo, uchaguzi mkuu matatani

Wafanyakazi wa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi huu nchini Mali wametangaza kuwa wamerefusha mgomo wao, suala ambalo limezusha wasiwasi kuhusu zoezi hilo la kidemokrasia ambalo lilitazamiwa kuhitimisha miaka sita ya machafuko ya kisiasa na mashambulizi yanayofanywa na makundi yenye misimamo mikali.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Taifa la Watendaji wa Serikali nchini Mali, Olivier Traore amesema kuwa jumuiya mbili ambazo kazi zao ni pamoja na kusambaza kadi za wapiga kura, zimerefusha mgomo wao. Amesema serikali ya Bamako imeshindwa kutimiza matakwa ya wafanyakazi hao katika muda uliokuwa umeainishwa wa tarehe Mosi Julai na kwamba mgomo huo utaathiri matayarisho ya uchaguzi wa tarehe 29 Julai.

Wafanyakazi wa uchaguzi mkuu wa Mali walianza mgomo huo tarehe 25 Juni wakilalamikia mazingira mabaya ya kazi na maisha magumu.

Ghasia na machafuko vimeshamiri nchini Mali

Kuna wasiwasi mkubwa juu ya uwezo wa serikali ya Mali wa kutayarisha zoezi huru na salama la uchaguzi kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya makundi ya waasi na ghasia zinazosababishwa na mivutano iliyopo kati ya makundi ya kikabila.

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya haki za binadamu, Alioune Tine ametahadharisha kuhusu hali ya usalama nchini Mali na kusema mashambulizi na mauaji vimeongezeka nchini humo katika siku za hivi karibuni.