Jul 27, 2018 07:47 UTC
  • Virusi vipya vya Ebola vyagunduliwa Sierra Leone

Serikali ya Sierra Leone imetangaza habari ya kungunduliwa virusi vipya ya ugonjwa hatari wa Ebola, miaka miwili baada ya maradhi hayo kusemekana kuwa yamemalizika kabisa nchini humo.

Amara Jambai, afisa wa ngazi za juu wa Wizara ya Afya nchini humo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, virusi hivyo vimegunduliwa kwa popo, na wataalamu wa afya wanasema vinaweza kusambazwa kutoka kwa mnyama huyo mdogo kipofu anayefanana na panya hadi kwa binadamu.

Kwa upande wake, Harold Thomas, msemaji wa Wizara ya Afya wa Sierra Leone amewataka wananchi kutokula nyama ya popo, kama hatua ya kwanza ya tahadhari, huku akiwataka wasubiri ripoti ya mwisho ya wataalamu wa afya nchini humo, kuhusu virusi hivyo.

Siku chache zilizopita, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitangaza rasmi kwamba maambukizi ya ugonjwa wa Ebola yamekomeshwa kikamilifu nchini humo.

Ebola

Machi mwaka 2016, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa, Sierra Leone imefanikiwa kuutokomeza ugonjwa hatari wa Ebola nchini humo.

Itakumbukwa kuwa, watu zaidi ya 11,000 walifariki dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa  wa Ebola katika eneo la Afrika Magharibi mwaka 2014 hadi 2015, hususan nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia katika mlipuko wa Ebola uliotajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani. 

Tags