Aug 17, 2018 04:08 UTC
  • Kambi ya upinzani Mali yapinga matokeo ya uchaguzi wa rais

Kambi ya upinzani nchini Mali imepinga matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa jana na kumpa ushindi Rais wa nchi hiyo, Ibrahim Boubacar Keïta.

Wafuasi wa aliyekuwa mpinzani wa Keita katika uchaguzi huo, Soumaïla Cissé wamesema kuwa watatumia njia zote za kidemokrasia kwa ajili ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyotangazwa jana. 

Kambi ya upinzani nchini Mali inasema matokeo yaliyotangazwa ya duru ya pili ya uchaguzi wa rais hayaoani na kura zilizopigwa na wananchi katika masanduku ya kupigia kura. 

Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanaonyesha kuwa, Rais anayemaliza muda wake nchini Mali, Ibrahim Boubacar Keita ameshinda duru ya pili ya uchaguzi wa urais kwa kupata asilimia 67.17 ya kura huku mpinzani wake, Soumaila Cissé akiambulia asilimia 32.83% ya kura zote.

Upinzani Mali wakataa matokeo ya uchaguzi wa rais

Akitangaza matokeo hayo, Mohamed Ag Erlaf, Waziri wa Masuala ya Utawala wa Mali amesema kuwa, Boubacar Keita ndiye mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi huo na kwamba ataiongoza nchi hiyo kwa miaka mingine mitano.

Ripoti zinasema kuwa, mawasiliano ya intaneti na mitandao ya kijamii yalikatwa jana katika mji mkuu wa Mali, Bamako baada ya kutangazwa rasmi matokeo ya uchaguzi wa rais.   

Tags