Aug 26, 2018 14:48 UTC
  • Maafa ya Ebola yaongezeka DRC

Idadi ya watu waliopoteza maisha yao kutokana na mfumuko mpya wa homa hatari ya Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imefikia watu 67 katika mwezi huu wa Agosti pekee.

Wizara ya Afya ya nchi hiyo imetangaza kuwa, tangu ulipofumuka upya ugonjwa wa Ebola tarehe Mosi mwezi huu wa Agosti katika mji wa Mangina mkoani Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC hadi hivi sasa, kuna kesi 105 za maambukizi ya ugonjwa huo zimeripotiwa na kesi 77 kati ya hizo zimethibitishwa kuwa ni za ugonjwa huo katika maabara ya tiba.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, kati ya kesi hizo 77, ni watu 11 tu ndio waliotibiwa na kupona, waliobakia wengine wote yaani watu 67 wamepoteza maisha.

Image Caption

 

Wizara hiyo ya afya ya DRC imesema, ina wasiwasi wa kuenea zaidi ugonjwa huo huku madawa ya kupambana nao yakiwa hayapatikani hasa katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi.

Hayo yameripotiwa katika hali ambayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikuwa limesema kuwa, mripuko mpya wa ugonjwa wa Ebola umeshadhibitiwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, lakini wakati huo huo likatahadharisha kwamba, kuna uwezekano wa kutokea kesi mpya, kutokana na mazingira magumu yanayosababishwa na hali mbaya ya usalama na kutofikika baadhi ya maeneo.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa idara ya dharura ya WHO Dr. Peter Salama alisema, mpaka kufikia siku ya Jumatano, tarehe 22 Agosti, 2018, idadi ya maambukizi haikuzidi 100, huku kesi 103 zikithibitishwa pamoja na vifo vya watu 63. Alisema mripuko wa hivi sasa wa Ebola umezikumba wilaya sita mkoani Kivu Kaskazini na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Ituri.

Tags