Shein ateua baraza la mawaziri, asema hatishwi na 'kelele' za CUF
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dakta Ali Mohamed Shein ametangaza Baraza la Mawaziri lenye wizara 13 huku akisema kuwa hababaishwi na hatua ya chama kikuu cha upinzani visiwani humo CUF kutoitambua serikali yake.
Baraza hilo lina sura mpya nane, likiwajumuisha wajumbe kutoka vyama vya siasa vya upinzani, wanasiasa mashuhuri visiwani humo, huku naibu mawaziri saba wote wakiwa wageni katika nafasi hiyo.
Akitangaza majina hayo jana, Dakta Shein anayeianza awamu ya pili ya utawala wake Zanzibar, alimtangaza Dakta Halid Salum Mohammed, ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Donge, kuwa Waziri wa Fedha na Mipango. Riziki Pembe Juma, Mwakilishi wa Viti Maalumu, ameteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, wakati Moudin Castico, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi aliyeteuliwa na Rais, anakuwa Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wazee, Wanawake na Watoto. Wengine ni Rashid Ali Juma, Mwakilishi wa Jimbo la Amani ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo. Balozi Amina Salum Ali aliyeshika nafasi ya pili, baada ya Rais John Magufuli, katika mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka jana, yeye ameteuliwa kuwa Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko. Shein amesema hababaishwi na kauli za CUF zilizotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif za kutoitambua serikali yake na kusisitiza Serikali yake inatambuliwa na Mungu ambaye ameipa baraka zote pamoja na wananchi wa Unguja na Pemba ambao ndiyo walioipigia kura kwa wingi na kuipa nafasi ya kushika hatamu ya madaraka.
Wakati huohuo Katibu Mkuu wa CUF leo anatazamiwa kufanya mkutano na waandishi wa habari kutangaza mustakabali na muelekeo wa chama hicho baada ya kususia uchaguzi mkuu wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu.../