Sep 01, 2018 14:07 UTC
  • WHO yasema hatua za kudhibti Ebola  DRC zinafanya kazi

Shirika la Afya Duniani WHO limesema huku hatua za kudhibiti ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zikitekelezwa, kuna hatari ya kuendelea kuenea ugonjwa huo.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa, hadi kufikia siku ya Jumatano watu 77 walikuwa wamefariki katika mlipuko mpya wa Ebola ulioanza Agosti Mosi katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mikoani Kivu Kaskazini na Ituri. Wastani wa umri wa waliofariki kwa Ebola na wanaodhaniwa kufa kwa ugonjwa huo ikiwa ni miaka 35 na asilimia 56 wakiwa ni wanawake.

Miongoni mwa wagonjwa walioripotiwa, 15 ni wafanyakazi wa afya, ambapo 14 walithibitika na mmoja alifariki. WHO na washirika wake wanafanya kazi na watumishi wa afya na jamii ili kuongeza elimu ya uelewa kuhusu kinga na hatua za kudhibiti, pamoja na chanjo kwa wale walio kwenye hatari kubwa.

Hatua za kudhibiti Ebola

Kwa mujibu wa WHO, kwa sasa hatua za kudhibiti Ebola zinafanya kazi. Katika kipindi cha wiki moja iliyopita, uwezo wa kutambua maambukizi umeongezeka, wagonjwa wengine kwa sasa wamefikishwa katika vituo vya matibabu ya Ebola kupata tiba saa chache baada ya kugundulika kuwa na Ebola, na shughuli za kutoa kinga zimefika katika maeneo mengi yaliyothibitika kuwa na wagonjwa wengi katika wiki tatu zilizopita. Hivyo WHO limeonya kuwa kusambaa kwa ugonjwa huo, lazima kufuatiliwe kwa tahadhari.

 

Tags