Rais wa Madagascar ajiuzulu ili kuwania urais mwezi Novemba
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47984-rais_wa_madagascar_ajiuzulu_ili_kuwania_urais_mwezi_novemba
Rais Hery Rajaonarimampianina wa Madagascar amejiuzulu, ili aweze kupata fursa ya kuwania urais kwa muhula wa pili mfululizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 08, 2018 10:51 UTC
  • Rais wa Madagascar ajiuzulu ili kuwania urais mwezi Novemba

Rais Hery Rajaonarimampianina wa Madagascar amejiuzulu, ili aweze kupata fursa ya kuwania urais kwa muhula wa pili mfululizo.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika tarehe 7 mwezi Novemba na kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, rais anatakiwa  kuachia madaraka mwezi mmoja kabla ya uchaguzi kufanyika.  Spika wa Bunge la Senate, Riko Rakotovao atachukua uongozi wa nchi kwa muda.

Rais huyo wa hivi sasa Madagasvar anaanza kampeni huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa marais wa zamani Didier Ratsiraka, Marc Ravalomanana na Andry Rajoelina.

Wapinzani hao watatu, walifungiwa kuwania urais mwaka 2013 na wanarejea na ahadi za kuimarisha uchumi wa kisiwa hicho na kuunda nafasi za ajira.

Andry Rajoelina                                                       Marc Ravalomanana 

Siku ya Jumatano Ratsiraka alisema uchaguzi wa hivi sasa unafanyika kinyume cha sheria kwani kuna ulazima wa kuwa na serikali ya mpito katika kipindi cha uchaguzi.

Mshindi wa uchaguzi huu ni lazima apate asilimia 50 ya kura zote, la sivyo kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi.

Madagascar ni kisiwa kilichoko kusini mwa bara la Afrika na idadi ya watu katika nchi hiyo ni milioni 25. Nchi hiyo ambayo ilikoloniwa na Ufaransa imekuwa ikishuhudia miongo mingi ya migogoro ya kisiasa na umasikini ya kupindukia.