Chama tawala chazoa viti vingi katika uchaguzi wa Bunge Mauritania
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Mauritania imetangaza habari ya kuibuka mshindi chama tawala nchini humo katika duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge iliyofanyika Septemba 15.
Ikitoa tangazo hilo jana Jumatatu, tume hiyo imesema chama hicho cha Union for the Republic kimejizolea viti 93 kati ya 157 vya Bunge la Kitaifa.
Kadhalika chama hicho tawala chake Rais Mohamed Ould Abdul Aziz kimeshinda viti vyote katika uchaguzi wa majimbo huku kikizoa manispaa 169 kati ya 219 katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Septemba Pili.
Uchaguzi wa rais nchini Mauritania unatazamiwa kufanyika katikati ya mwaka 2019, na kuibuka mshindi chama tawala katika uchaguzi wa Bunge, majimbo na serikali za mitaa, ni bishara njema kwa Rais Abdul Aziz.
Itakumbukwa kuwa, Agosti mwaka jana, wananchi wa Mauritania walipasisha kwa wingi wa kura marekebisho ya Katiba ya nchi hiyo kupitia kura ya maoni.
Miongoni mwa marekebisho hayo ni kufutwa Bunge la Seneti na nafasi yake kuchukuliwa na Mabaraza ya Kieneo, mbali na kufutwa Mahakama ya Juu ya Uadilifu na kufanyiwa mabadiliko pia bendera na wimbo wa taifa wa nchi hiyo.