Al Azhar ya Misri yasisitiza kufanyika mazungumzo kati ya dini za mbinguni
Sheikhul Azhar wa Misri amesisitiza juu ya ulazima wa kufanyika mazungumzo kati ya dini za mbinguni kwa minajili ya kukurubisha pamoja fikra na mitazamo kati ya dini hizo.
Sheikh Ahmad al Tayyeb amesema kuwa upo udharura wa kufanyika mazungumzo kati ya dini za mbinguni. Amaeyasema hayo alipokutana na Volker Kauder Mkuu wa Mrengo wa Chama cha Demokrasia cha Kikristo katika bunge la Ujerumani.
Sheikhh Ahmad al Tayyeb ameongeza kuwa dini za Mwenyezi Mungu hazijabainishwa kwa ajili ya kutenda ukatili, na kwa msingi huo kundi dogo lenye misimamo ya kuchupa mipaka halipasi kuarifishwa kama kundi la Kiislamu. Amesema kuwa watu wa aina hii wanatekeleza vitendo vya kipekee na tofauti kabisa ambavyo havina uhusiano wowote na dini ya Kiislamu.
Ahmad al Tayyeb ameashiria juhudi za Chuo Kikuu cha kidini cha al Azhar cha Misri katika mapambano dhidi ya fikra potofu na kueleza kuwa, Chuo hicho hivi sasa kimeweka katika ajenda yake ya kazi mpango wa kuwatuma wahubiri kote nchini humo ili kuwalinda vijana mkabala na misimamo na fikra hizo kinzani. Shekhe Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kidini cha al Azhar amesisitiza pia kuwa, chuo hicho kimeanzisha "msafara wa amani na urafiki" katika ngazi ya kimataifga na kwa kushirikiana na Baraza Kuu la Waislamu kwa lengo la kueneza utamaduni wa Kiislamu baina ya mataifa ya dunia.