Umoja wa Mataifa wataka kufanyike uchunguzi kuhusu mauaji ya waandamanaji Sudan
Umoja wa Mataifa umelezea kusikitishwa sana na machafuko pamoja na mauaji ya waandamanaji nchini Sudan na umewataka viongozi wa nchi hiyo wafanye uchunguzi unaotakiwa wa kubaini kwa nini waandamanaji wanauawa.
Kitengo cha upashaji habari cha Umoja wa Mataifa kimemnukuu msemaji wa umoja huo Stéphane Dujarric, akisema hayo na kuongeza kuwa, Katibu Mkuu wa umoja huo António Guterres ametaka kudumishwe utulivu nchini Sudan na kutotumiwa nguvu katika kukabiliana na waandanaji.
Vile vile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mkono wa pole kwa familia za watu waliouawa hivi karibuni katika maandamano ya Sudan na kuhimiza kuheshimiwa misingi ya uhuru wa kusema na kuitisha mikusanyiko ya amani nchini humo.
Makumi ya miji ya Sudan ukiwemo Khartoum, mji mkuu wa nchi hiyo inashuhudia maandamano makubwa ya wananchi tangu Jumatano ya wiki iliyopita ya tarehe 19 Disemba kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu hasa mkate na mafuta.
Taarifa zinasema kuwa Sudan haijawahi kukumbwa na maandamano makubwa kiasi hicho katika kipindi cha miaka 30 iliyopita na hadi hivi sasa watu 38 wameshauliwa na maafisa usalama wa serikai ya Rais Omar al Bashir. Waandamanaji hao wanataka serikali ya al Bashir ing'olewe madarakani.
Serikali ya Sudan imetangaza hali ya hatari katika baadhi ya mikoa ukiwemo wa Khartoum na kufunga shule na vyuo vikuu vikiwemo vya mji mkuu huo wa Sudan.