Wahajiri 14 wa Ethiopia waaga dunia katika mazingira ya kutatanisha Tanzania
Polisi ya Tanzania imetangaza habari ya kuaga dunia wahamiaji 14 waliothibitishwa kuwa raia wa Ethiopia mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania.
Shirika la habari la Xinhua limemnukuu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa, akisema wahamiaji hao waligunduliwa kufa ndani ya gari dogo katika eneo la Mindu, katika barabara kuu ya Tanzania kuelekea Zambia.
Amesema gari hilo lilikuwa na wahamiaji 26 haramu waliokuwa na nia ya kuelekea Afrika Kusini, na kwamba watano miongoni mwao wamepelekwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya.
Ofisa wa afya wa Morogoro Francis Semwene amesema chanzo cha vifo hivyo ni kujazana wahamiaji hao kupindukia kwenye gari dogo, lisilokuwa na uwezo wa kubeba watu 26.
Kwa upande wake, ofisa wa uhamiaji wa eneo hilo, Safina Mhindi amesema kufikia sasa haijabainika iwapo miili ya wahajiri hao itazikwa nchini Tanzania au itasafarishwa nchini Ethiopia.
Tanzania inahesabiwa kuwa njia kuu kwa wahamiaji haramu wanaotaka kwenda nchini Afrika Kusini kusaka ajira na maisha mazuri.