Amnesty: Ukandamizaji umefikia kileleni Misri katika utawala wa al Sisi
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeripoti kuwa, ukandamizaji wa haki ya kujieleza umefikia kileleni katika kipindi cha utawala wa Rais wa sasa wa Misri, Abbel Fattah al Sisi.
Taarifa ya Amnesty International imesema kuwa, hali inayotawala sasa nchini Misri ni tofauti kabisa na madai yaliyotolewa na Rais wa nchi hiyo aliyedai kuwa, hakuna mfungwa wa kisiasa huko Misri.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesisitiza kuwa, kuna wafungwa elfu sitini wa kisiasa nchini Misri kutokana na ukandamizaji mkubwa unaoendelea tangu baada ya mapinduzi ya Julai 2013 yaliyoiondoa madarakani serikari halali ya Rais Muhammad Morsi.
Ukandamizaji huo unalenga zaidi wanachama wa harakati ya Ikhwanul Muslimin, waandishi habari, watetezi wa haki za binadamu, wanasheria na hata maafisa wa taasisi za michezo.

Amnesty International imeongeza kuwa, kuikosoa serikali ya sasa ya Misri ni hatari kubwa kwa wanaharakati kuliko wakati wowote mwingine katika historia ya nchi hiyo. Imeongeza kuwa, Wamisri wanaoeleza maoni yao kwa njia ya amani hutambuliwa kuwa ni wahalifu katika serikali Abdul Fattah al Sisi na kwamba Misri imekuwa kama jela ya wazi kwa wakosoaji wa utawala huo.