CAR yahitaji dola milioni 430 kuwasaidia wananchi 2019
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50722-car_yahitaji_dola_milioni_430_kuwasaidia_wananchi_2019
Jamhuri ya Afrika ya kati, CAR inaendelea kukabiliwa na janga la kibinadamu ambapo mtu mmoja kati ya wanne ni mkimbizi wa ndani au nje ya nchi, imesema Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 08, 2019 03:48 UTC
  • CAR yahitaji dola milioni 430 kuwasaidia wananchi 2019

Jamhuri ya Afrika ya kati, CAR inaendelea kukabiliwa na janga la kibinadamu ambapo mtu mmoja kati ya wanne ni mkimbizi wa ndani au nje ya nchi, imesema Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, OCHA.

OCHA katika taarifa iliyotolewa Jumatatu huko Bangui, mji mkuu wa CAR, imesema idadi ya watu wanaohitaji msaada na ulinzi mwaka huu imeongezeka kutoka watu milioni 2.5 hadi 2.9 ikiwa ni ongezeko la asilimia 16 ikilinganishwa na mwaka 2018.

Kati ya hao, watu milioni 1.9 wanahitaji msaada wa dharura na haraka.

Kwa mantiki hiyo OCHA kwa pamoja na serikali ya CAR, imetoa ombi kwa ajili ya mpango wa msaada kwa mwaka 2019 la dola milioni 430.7 kusaidia watu milioni 1.7 walio hatarini zaidi nchini CAR.

Kwa kuzingatia malengo matatu, mpango huo unatarajiwa kuokoa maisha, kuimarisha ulinzi wa watu walioathirika na wakati huo huo kuwezesha utoaji wa huduma muhimu za kuokoa maisha.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati

Machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliibuka mwaka 2013 baada ya waasi wa Seleka kumuondoka madarakani aliyekuwa rais wa taifa hilo, François Bozizé, huku mgogoro ukishadidi zaidi baada ya waasi wa Kikristo wenye kufurutu ada wa Anti-Balaka kuanzisha mauaji ya kutisha dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya watu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi. 

Hivi sasa kuna askari 10,000 wa kulinda amani katika nchi hiyo iliyo kati kati mwa bara la Afrika lakini hawajaweza kutuliza hali ya mambo na mapigano ya hapa na pale yangali yanaendelea.