Afrika Kusini kupunguza uhusiano wake na Israel, yawaunga mkono Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52055-afrika_kusini_kupunguza_uhusiano_wake_na_israel_yawaunga_mkono_wapalestina
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa nchi yake inapanga kupunguza hadhi ya ubalozi wake katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina kutokana na ukiukaji wa haki za Wapalestina unaofanywa na utawala haramu wa Israel.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Mar 09, 2019 11:45 UTC
  • Afrika Kusini kupunguza uhusiano wake na Israel, yawaunga mkono Wapalestina

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema kuwa nchi yake inapanga kupunguza hadhi ya ubalozi wake katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina kutokana na ukiukaji wa haki za Wapalestina unaofanywa na utawala haramu wa Israel.

Rais Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye alikuwa akihutubia Bunge la nchi hiyo amesema kuwa, Waziri wa Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa wa nchi hiyo, Lindiwe Sisulu anafanya mikakati ya kutekeleza uamuzi uliochukuliwa na chama tawala cha African National Congress (ANC) wa kupunguza uhusiano wa kidiplomasia na Israel.

Katika mkutano wake wa Disemba 2017, chama cha ANC kilichukua uamuzi wa kupunguza kiwango cha hadhi ya ubalozi wake mjini Tel Aviv na kuwa na ofisi ya mawasiliano, kama hatua ya kuonesha uungaji mkono wa Pretoria kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.  Afrika Kusini pia ilitahadharisha kuwa, Israel italipa gharama kubwa kutokana na ukiukaji wake wa haki za binadamu na sheria za kimataifa.

Rais wa Afrika Kusini amesisitiza kuwa, serikali yake itatekeleza maamuzi ya chama tawala cha ANC.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini 

Mwezi Mei mwaka jana pia Afrika Kusini ilimrejesha nyumbani balozi wake huko Tel Aviv ikilalamikia ukandamizaji na mauaji yanayofanywa na jeshi la Israel dhidi ya raia wanaoandamana katika Ukanda wa gaza.

Raia wengi wa Afrika Kusini wamekuwa wakiliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina kutokana na mfanano uliopo baina ya utawala haramu wa Israel na ule uliokuwa ukitawala kwa misingi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.