Wachimba migodi 5 wauawa katika eneo la Oromia, Ethiopia
Watu waliobeba silaha wameshambulia timbo (mgodi) na kuua wachimba migodi watano katika eneo la Oromia magharibi mwa Ethiopia.
Shirika la habari la serikali nchini humo Fana limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, mauaji hayo yalifanyika jana Jumanne baada ya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia kampuni ya kuchimba migodi karibu na mji wa Nedjo, umbali wa kilomita 500 toka mji mkuu Addis Ababa, magharibi mwa nchi.
Shirika la habari la Reuters limenukuu mashuhuda wa tukio hilo wakisema kuwa, watu hao waliokuwa wamebeba silaha waliingia ndani ya kampuni hiyo na kuanza kufyatia risasi ovyo, ambapo watu watano wameuwa huku wengine kadhaa wakijeruiwa.
Inaarifiwa kuwa, raia wawili wa kigeni ni miongoni mwa wachimba migodi waliouawa katika hujuma hiyo ya jana Jumanne.
Aghalabu ya wakazi wa eneo la Oromia lililoko magharibi mwa Ethiopia ni watu wa kabila la Oromo.
Kundi la Harakati ya Ukombozi ya Oromo linalokadiriwa kuwa na maelfu ya wapiganaji wakiwa sehemu ya magharibi ya jimbo la Oromia, katika miezi ya hivi karibuni limekuwa likifanya mashambulizi dhidi ya jeshi na raia. Machafuko katika eneo la Oromia yalianza mwaka 2015 baada ya kutekwa ardhi za wakulima na matajiri wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.