Sudan yaendelea kugubikwa na maandamano ya kumtaka Rais al-Bashir aachie madaraka
Maandamano ya kupinga serikali ya Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan yameendelea kushuhudiwa katikak miji mbalimbali ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Khartoum.
Katika maandamano yaliyofanyika jana, zaidi ya Wilaya 20 za mji mkuu Khartoum zilishuhudia maandamano huku waandamanaji wakipiga nara dhidi ya Rais Omar Hassan al-Bashir na chama tawala cha National Congress Party.
Aidhaa maandamano kama hayo yameshuhudiwa pia katika miji mingine ya Sudan ukiwemo mji wa Omdurman.
Tangu katikati ya mwezi Desemba mwaka jana hadi sasa, Sudan imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa ya kulalamikia hali mbaya ya uchumi na ongezeko la bei za bidhaa.
Maandamano ya hivi sasa ya nchini Sudan ni makubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Maandamano hayo yaliyoanza kwa kulalamikia ughali wa maisha yamebadilika na kuwa wimbi la kumtaka Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo ang'oke madarakani, lakini bado anashikilia msimamo wake wa kubakia uongozini.
Makumi ya waandamanaji ambao wanataka Rais Omar al-Bashir ang'atuke madarakani wametiwa mbaroni, huku ripoti za asasi za kiraia zikieleza kuwa watu zaidi ya watu 50 wameuawa hadi sasa katika ghasia na machafuko huko Sudan.
licha ya kutangazwa hali ya hatari na hata kuundwa baraza jipya la mawaziri, yote hayo hayajafanikiwa kutuliza mambo mambo kwani maandamano hayo yameendelea kushuhudiwa karibu kila siku nchini Sudan.