Waliofariki dunia katika Kimbunga Idai wafika 746, maelfu wapoteza makazi
Mamia ya maelfu ya watu wanahitaji misaada ya dharura ya chakula, maji na makazi baada ya Kimbunga Idai kusababisha uharibifu mkubwa Msumbiji, Zimbabwe na Malawi.
Hadi kufikia Jumamosi ya leo, watu wasiopungua 746 walikuwa wamethibitishwa kupoteza maisha katika kimbunga hicho ambacho kiliandamana na mvua kali pamoja na mafuriko.
Kimbunga Idai kilifika katika Bandari ya Beira nchini Msumbuji Machi 14 ambapo kiliandamana na upepo mkali na kupelekea mito miwili mikubwa ya Buzi na Pungua kuvunja kingo na kufurika vijiji kadhaa. Kwa uchache watu 501 walipoteza maisha Msumbiji huku nyumba karibu laki moja zikiharibiwa. Mnamo Machi 16 Kimbunga Idai kilifika mashariki mwa Zimbabwe na kupelekea watu 259 kupoteza maisha mbali na kusababisha hasara kubwa katika wilaya za Chimanimani na Chipinge. Kimbunga Idai pia kilifika katika nchi jirani ya Malawi katika wilaya za Chikwawa na Nsanji na kupelekea watu wasiopungua 60 kupoteza maisha mbali na kusababisha hasara kubwa.

Kufuatia hali hiyo, mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa umetangaza kutoa msaada wa dola milioni 20 kusaidia waathirika.
Kwa mujibu wa mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Mark Lowcock mfuko huo wa dharura CERF umetangaza kutenga dola milioni 20 kwa ajili ya kupiga jeki msaada wa kibinadamu kufuatia Kimbunga Idai kilichokumba nchi hizo tatu za kusini mwa Afrika.
Lowcock hata hivyo amesema mgao huo kutoka kwa CERF ni wa kukabiliana na dharura za hivi sasa lakini hautoshi kuweza kukabiliana na mahitaji ambayo yanatarajiwa kuongezeka na hiyvo ametoa wito kwa wafadhili kuchangia fedha kwa ajili ya watu walioathirka kufuatia kupiga kwa kimbunga Idai.