Mapinduzi nchini Sudan, kupanuka mgogoro wa kisiasa
Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan umeingia katika hatua mpya, kufuatia mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Omar Hassan al-Bashir Rais wa nchi hiyo na kuchukua jeshi hilo hatamu za uongozi wa nchi hiyo.
Jeshi la Sudan limechukua hatamu za uongozi nchini Sudan baada ya mapinduzi ya ghafla ambapo Jenerali Awad Mohamed Ahmad Ibn Auf, Waziri wa Ulinzi wa Sudan aliteuliwa kuwa Kaimu Rais. Hata hivyo siku moja tu baada ya kuapishwa kuchukua wadhifa huo, Jeneralii Ibn Auf ametangaza kujiuzulu, baada ya makumi ya maelfu ya Wasudani kuendeleza maandamano wakitaka kuweko makabidhiano ya kiraia ya uongozi. Mapinduzi ya kijeshi yametokea nchini Sudan baada ya miezi kadhaa ya maandamano ya wananchi ambayo awali yalikuwa yakilalamikia ughali wa maisha kabla ya kuchukua mkondo wa kisiasa.
Maandamano hayo yalichukua mkondo mpana zaidi baada ya vyama na makundi ya kisiasa kujiunga nayo na kutangaza wazi matakwa yao kama kuweko uhuru wa kiraia, kisiasa, kijamii na kidemokrasia. Kwa miezi kadhaa waandamanajji nchini Sudan walikuwa wakitaka kujiuzulu Omar Hassan al-Bashir, kuundwa serikali ya mpito na kisha kufanyika uchaguzi katika anga uhuru na ya kidemokrasia.
Licha ya kuwa katika muda wote huo wa maandamano Omar al-Bashir alifanya kila awezalo kuhakikisha anabakia madarakani na kuchukua hatua kama za kufanya mabadiliko ya kidhahiri na kuimarisha hatua za kiusalama sambamba na kutekeleza siasa za ukandamizaji kwa ajili ya kuzusha wofu na woga miongoni mwa wananchi, lakini yote hayo hayakuwa na natija na badala yake yalipelekea kushadidi malalamiko na maandamano ya wananchi.
Hivi sasa Baraza la Kijeshi la Mpito linaloshikilia hatamu za uongozi nchini Sudan limetangaza kuwa, litaboresha hali ya mambo na kuandaa mazingira ya kukabidhi madaraka kwa njia ya demokrasia. Licha ya tangazo hilo la Baraza la Kijeshi la Mpito, waandamanaji nchini Sudan wametangaza kuwa, wataendelea na maandamano na malalamiko yao hadi pale matakwa yao likiwemo suala la kukabidhiwa uongozi kwa utawala wa kiraia yatakapotekezwa.
Makundi na vyama vingi vya kisiasa nchini Sudan navyo vinaamini kuwa, mapinduzi hayo ya kijeshi sio mabadiliko ya kimsingi bali ni mabadiliko ya uongozi wa juu tu, ambayo katu hayawezi kuwa na taathira yoyote chanya kwa ufumbuzi wa kisiasa na matatizo ya kiuchumi ya wananchi.
Jumuiya ya Wafanyakazi nchini Sudan imetangaza kuwa, kile ambacho kimetokea nchini humo ni mapinduzi mapya yenye lengo la kuvuruga hali ya mambo na kwamba, jumuiya hiyo itaendeleza maaandamano na malalamiko ili kuhakikisha kuwa, kunafanyika uchaguzi utakayoyajumuisha makundi yote.
Filihali hali ya mambo na mazingira yanayotawala katika nchi hiyo ni tata zaidi. Akthari ya raia wana wasiwasi na kuundika tena mfumo wa utawala wa kijeshi katika nchi hiyo. Wajuzi wa mambo wanasema kuwa, kufanyika mapinduzi ya kijeshi huko Sudan na Baraza la Kijeshi kuchukua uongozi wa mpito kunatia wasiwasi wa kuhuika tena nguvu na utawala wa kijeshi.
Akthari ya waandamanaji wanaamini kuwa, sera za Omar al-Bashir ziliandaa uwanja wa kuweko uingiiliaji wa kigeni zaidi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Ukweli wa mambo ni kuwa, Sudan imegeukka na kuwa mahala pa kujidhihirisha madola ya kigeni hususan Marekani, utawala haramu wa Israel na washirika wake wa kieneo.
Ni kwa kuzingatiwa ukweli huo, ndio maana kuhitimisha uingiliaji wa kigeni wa kidhahiri na wa siri katika masuala ya ndani ya Sudan na kuingia madarakani serikali yenye ridhaa na baraka za wananchi ni matakwa mengine ya wananchi wa nchi hiyo.
Hapana shaka kuwa, siku za usoni za Sudan zitakuwa na hatima kwa mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo. Je Sudan itarejea upande wa utawala wenye ridhaa na kura za wananchi au kwa mara nyingine tena wanajeshi watashika hatamu za uongozi wa nchi na kuifanya nchi hiyo iendelee kuwa na ombwe la kidemokrasia na mahala pa madola ya kigeni kunufaika kisiasa na kiuchumi?