IEA: Kenya na Uganda zinatakatisha 'fedha chafu' za Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53006-iea_kenya_na_uganda_zinatakatisha_'fedha_chafu'_za_sudan_kusini
Ripoti ya Taasisi ya Masuala ya Uchumi IEA imefichua kuwa, Kenya na Uganda zimefeli kuzuia mzunguko wa pesa haramu zinazotoka katika nchi changa zaidi barani Afrika, Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2019 23:00 UTC
  • IEA: Kenya na Uganda zinatakatisha 'fedha chafu' za Sudan Kusini

Ripoti ya Taasisi ya Masuala ya Uchumi IEA imefichua kuwa, Kenya na Uganda zimefeli kuzuia mzunguko wa pesa haramu zinazotoka katika nchi changa zaidi barani Afrika, Sudan Kusini.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa, serikali za Nairobi na Kampala zinajiweka katika hatari ya kukabiliwa na vikwazo vya vyombo vya kimataifa vya kudhibiti mzunguko wa fedha, kwa kuruhusu chumi zao zichafuliwe na pesa hizo haramu kutoka Sudan Kusini.

IEA imesema Sudan Kusini imepoteza zaidi ya dola bilioni 6.8 katika kipindi cha miaka saba iliyopita, kutokana na mzunguko haramu na ufuaji wa fedha zake.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya ya Taasisi ya Masuala ya Uchumi, utakatishaji wa fedha chafu za Sudan Kusini umepanua zaidi mgogoro wa kisiasa na kibinadamu katika nchi hiyo.

Kenya na Uganda zatuhumiwa kuwa hifadhi ya pesa chafu za S/Kusini

Nairobi na Kampala zimetajwa kuwa hifadhi ya fedha hizo zinazoripotiwa kuingizwa katika nchi hizo za Afrika Mashariki kupitia maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi na wa kisiasa wa Sudan Kusini. 

Vita vya ndani nchini Sudan Kusini vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.

Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.