Watu 37 waaga dunia baada ya boti kuzama DRC
Miili 37 imepatikana baada ya boti nyingine kuzama huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wiki moja baada ya makumi ya watu kupoteza maisha huku wengine wengi wakitoweka baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Kivu katika mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa nchi.
Kaimu Gavana wa mkoa wa Maniema, Papy Omeonga Tchopa jana Jumanne aliliambia shirika la habari la AFP kuwa, boti hiyo ilizama katika kijiji cha Katalama, umbali wa kilomita 120 kutoka makao makuu ya mkoa huo, Kindu.
Amesema, "Boti hiyo ilizama mtoni mnamo Aprili 9. Tumepata miili 37 na tayari tumeizika. Tuliwakuta watu 16 walionusurika kwenye ajali hiyo karibu na eneo la ajali mashariki mwa nchi."
Afisa huyo wa serikali ameonya kuwa, maeneo ya Kindu, Kibombo na Kasongo ya mto huo hayapitiki na ni bora kwa wasafiri wanaoutumia boti hizo dhaifu kujieusha na maeneo hayo.

Katika ajali ya Aprili 15 katika Ziwa Kivu wakati wa safari ya Goma kuelekea Kalehe, watu zaidi ya 25 walithibitishwa kupoteza maisha huku wengine zaidi ya 100 wakitoweka.
Ajali za boti zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara DRC, na sababu kuu ya ajali hizo ni boti kujaza watu kupita kiasi na ubovu wa boti zenyewe. Mei mwaka jana, watu 49 walipoteza maisha baada ya boti kuzama mtoni kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.