Onyo la Baraza la Kijeshi la Sudan kwa wapinzani
Naibu mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan amesema kuwa kuna wanachama wa makundi ya wabeba silaha wanaoshiriki katika maandamano yanayoendelea nchini Sudan dhidi ya baraza hilo na kuonya kwamba subira ya baraza hilo ina mwisho wake.
Ikiripoti habari hiyo televisheni ya al-Jazeera imemnukuu Muhamed Hamdan Daqlu akisema kwamba Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan limewasilisha njia nyingi za kulindwa usalama katika jamii ya Sudan lakini akaongeza kwamba subira ya baraza hilo ina mipaka. Naibu mkuu huyo wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan amesema kuwa utawala wa nchi hiyo utakabidhiwa Baraza la Utawala ambalo litabuniwa hivi karibuni. Huku akisema kwamba katika kipindi chote cha historia ya mwanadamu hakujawahi kuripotiwa tukio la kushiriki wanajeshi na raia wa kawaida katika baraza moja, Daqlu amesisitiza kwamba wanajeshi ni sehemu ya harakati za wananchi na kwamba kuna vijana wengi walio pembeni yao.
Mohamed Hamdan Daqlu ameutuhumu Muungano wa Uhuru na Mabadiliko kwamba unafuatilia matakwa yasiyo ya kisheria ambayo hayakupitishwa katika kikao cha pande mbili na kusema kuwa msimamo wa muungano huo hauaminiki.
Baada ya kumpindua Rais Omar al-Bashir wa Sudan tarehe 11 mwezi Aprili, Baraza la Kijeshi la Mpito lilibuniwa na kuchukua madaraka ya nchi hiyo, lakini wanachi wamekuwa wakifanya maandamano ya kutaka madaraka hayo yakabidhiwe raia kutoka mikononi mwa wanajeshi. Hali hiyo imeongeza mvutano kati ya baraza hilo na wananchi wanaofanya maandamano kila siku nchini wakitaka wakabidhiwe madaraka haraka iwezekanavyo.