UN: 60% ya wananchi wa Sudan Kusini wanakabiliwa na baa la njaa
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema jumla ya watu milioni 7 sawa na asilimia 60 ya jamii nzima ya Sudan Kusini wanakabiliwa na baa la njaa.
Ripoti mpya ya serikali ya Sudan Kusini na mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa jana Ijumaa imebainisha kuwa, mbali na mapigano, mambo mengine yaliyosababisha nchi hiyo kukabaliwa na njaa kali ni mgogoro wa kiuchumi na kutoshuhudiwa mvua kwa kipindi kirefu.
Kwa mujibu wa mashirika hayo ya UN, zaidi ya theluthi mbili ya jamii nzima ya watu wa Sudan Kusini wanahitaji misaada ya chakula ili kukabiliana na njaa.
Hsiao-Wei Lee, afisa wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) amesema "Kila mwaka, baa la njaa nchini Sudan Kusini huongezeka kwa kiwango cha kutisha kiasi kwamba, mamilioni ya watu wa nchi hiyo hawajui mlo ujao utatoka wapi, hususan katika kipindi hiki cha kati ya mwezi Mei na Julai, ambapo kiwango cha njaa huwa kileleni."

Mashirika hayo ya UN ya WFP, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Mfuko wa Watoto wa umoja huo Unicef yamesema karibu watu milioni 1.8 wa Sudan Kusini wako katika kiwango cha 4 au kiwango cha 'hatari' cha kuandamwa na njaa na utapiamlo, na wanahitaji msaada wa dharura wa chakula.
Hivi karibuni, shirika la WFP lilitangaza kuwa, machafuko yanayoendelea nchini Sudan Kusini yanazuia operesheni za kugawa misaada ya chakula kwa watu wanaosumbuliwa na njaa kali katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.