Wimbi la tatu la mapinduzi na maandamano laanza Sudan
Muungano kwa jina la "Uhuru na Mabadiliko" unaolipinga Baraza la Kijeshi la Mpito linaloongoza Sudan umetangaza kuanza wimbi la tatu la mapinduzi na kurejea maandamano ya kila wiki nchini humo.
Muungano huo umetangaza kuanza wimbi la tatu la mapinduzi kwa kuzingatia kuwa Baraza la Kijeshi la Mpito limeshindwa kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia na wala hauna nia yoyote ya kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na mauaji ya waaandamanaji huko Khartoum tarehe Tatu mwezi huu. Muungano wa Uhuru na Mabadiliko umeongeza kuwa kila wiki kutakuwa kukifanyika maandamano ya nchi nzima kwa mujibu wa jedwali lililoainishwa.
Taarifa ya muungano huo unaolipinga baraza la uongozi wa kijeshi la Sudan imesisitiza kuwa maandamano yataendelea hadi itakapoundwa serikali ya kiraia. Umesema jumuiya ya wafanyakazi Alhamisi wiki ijayo itafanya maandamano makubwa huko Khartoum na katika miji mingine ya Sudan kulaani mauaji ya Juni tatu. Wanajeshi walichukua hatamu za uongozi Sudan baada ya kupinduliwa rais wa nchi hiyo Omar Hassan al Bashir tarehe 11 Aprili mwaka huu, hata hivyo wananchi na makundi ya kisiasa na kijamii yanaendelea kusisitiza kuundwa serikali ya kiraia nchini humo. Tarehe Tatu mwezi huu wa Juni jeshi la Sudan liliua watu 118 walokuwa wamekusanyika mbele ya makao makuu ya jeshi katika mji mkuu Khartoum.