Rais wa Misri kotini kwa kuipa Saudia visiwa vya Sanafir na Tiran
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5437-rais_wa_misri_kotini_kwa_kuipa_saudia_visiwa_vya_sanafir_na_tiran
Chama kimoja cha upinzani nchini Misri kimempelekea mahakamani Rais Abdul Fattah al-Sisi wa nchi hiyo kufuatia uamuzi wake wa kukabidhi umiliki wa visiwa viwili vya kiistratejia kwa utawala wa Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2016 03:13 UTC
  • Rais wa Misri kotini kwa kuipa Saudia visiwa vya Sanafir na Tiran

Chama kimoja cha upinzani nchini Misri kimempelekea mahakamani Rais Abdul Fattah al-Sisi wa nchi hiyo kufuatia uamuzi wake wa kukabidhi umiliki wa visiwa viwili vya kiistratejia kwa utawala wa Saudi Arabia.

Hamdeen Sabahi, kinara wa chama cha Popular Front amewasilisha mahakamani kesi yenye kurasa 10 kupinga uamuzi wa serikali ya Cairo kuipa Riyadh umiliki wa visiwa vya Sanafir na Tiran, vilivyoko katika Bahari Nyekundu nchini humo. Sabahi amesema ana nyaraka zinazotoa ithibati kuwa visiwa hivyo ni milki ya Misri na kwamba kukabidhi visiwa hivyo muhimu kwa nchi nyingine ni ukiukaji wa katiba na kukanyaga uhuru wa kujitawala. Haya yanajiri katika hali ambayo, wakili na mwanaharakati mwingine wa upinzani nchini humo Khalid Ali tayari ameipeleka mahakamani serikali ya Cairo kwa kuipa Saudia visiwa hivyo. Wakati huo huo, mwanaharakati mwingine mashuhuri ambaye pia ni mtafiti wa nchini Misri anayeishi nchini Ujerumani, Taqadum Al-khatib ameliambia gazeti la As-Safir linalochapishwa mjini Bairut nchini Lebanon kuwa, ramani iliyoko katika maktaba ya mjini Berlin, Ujerumani na kadhalika ramani zote za dunia, zinathibitisha wazi kwamba, visiwa hivyo viwili vya Sanafir na Tiran vilivyoko katika Ghuba ya Aqaba ni mali ya Misri na sio Saudia. Hivi karibuni Rais Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri alimpatia Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudia visiwa vya Sanafir na Tiran na kudai kuwa, michoro ya kimipaka baharini inaonyesha kwamba, visiwa hivyo vilivyoko Bahari Nyekundu viko katika maji ya Saudia.