Nchi za Afrika Magharibi kuzindua sarafu ya pamoja itakayoitwa 'ECO'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54458-nchi_za_afrika_magharibi_kuzindua_sarafu_ya_pamoja_itakayoitwa_'eco'
Nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) zimeafikiana kuiita sarafu mpya itakayotumiwa na nchi hizo 'ECO'.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jun 30, 2019 03:17 UTC
  • Nchi za Afrika Magharibi kuzindua sarafu ya pamoja itakayoitwa 'ECO'

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) zimeafikiana kuiita sarafu mpya itakayotumiwa na nchi hizo 'ECO'.

Sarafu hiyo inatazamiwa kuzinduliwa mwaka ujao wa 2020. Hayo yameafikiwa katika kikao cha nchi 15 wanachama wa ECOWAS kilichofanyika jana Jumamosi katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja.

Baadhi ya majina ya sarafu hiyo ambayo yalikuwa yamependekezwa hapo awali lakini yakakataliwa na nchi wanachama ni "Afri" na "Kola". 

Wachumi wameifananisha sarafu hiyo ya ECO na EURO ya nchi za Ulaya, na wanasema kuwa itatoa machango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na mabadilishano ya kibiashara miongoni mwa nchi wanachama. 

Viongozi wa Ecowas katika mkutano wa mwaka jana nchini Togo

Hivi sasa nchi nane wanachama wa ECOWAS Benin, Burkina Faso, Guinea-Bissau, Ivory Coast, Mali, Niger, Senegal na Togo zinatumia Franca ya Afrika Magharibi CFA.

Nchi saba zilizosalia wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika ambazo ni Cape Verde, Gambia, Ghana, Guinea, Liberia, Nigeria na Sierra Leon zina sarafu zao kila mmoja.