Maandamano ya wananchi wa Algeria yaendelea chini ya ulinzi mkali
Maelfu ya wananchi wa Algeria wanaendelea na maandamano yao ya nchi nzima chini ya ulinzi mkali kushinikiza kufukuzwa serikalini mabaki yote ya utawala wa Abdulaziz Bouteflika, rais wa nchi hiyo aliyelazimika kujiuzulu kutokana na maandamano makubwa ya wananchi.
Wananchi wa Algeria jana Ijumaa waliendelea na maandamano yao ya kila wiki ikiwa ni Ijumaa ya 20 mfufulizo wakipiga nara za kulaani majenerali wa kijeshi na kuwataka waache kuwaunga mkono na kuwasaidia mabaki ya utawala wa Abdulaziz Bouteflika.
Wananchi wengi walijiunga na maandamano hayo kutoka misikitini na majumbani ili kuwathibitishia wanajeshi kwamba, lengo lao ni kung'olewa kabisa wafuasi wa rais wa zamani wa nchi hiyo na kuundwa serikali huru ya kidemokrasia itakayohudumia raia.
Maandamano hayo yamefanyika sambamba na maadhimisho ya mwaka wa 57 wa uhuru wa Algeria kutoka kwa mkoloni Ufaransa. Wananchi walitumia fursa hiyo kupiga nara na mayowe ya kutaka utawala wa wananchi, kupigwa vita ufisadi, kupambana na wizi serikalini na kufukuzwa mabaki yote ya Abdulaziz Bouteflika.
Tarehe pili Aprili mwaka huu, Abdula Aziz Bouteflika alilazimika kuachia madaraka ya Algeria baada ya kushadidi maandamano ya wananchi.
Madaraka ya Algeria hivi sasa yako mikononi mwa Abdul Qadir bin Saleh, Spika wa Bunge la nchi hiyo ambaye anaongoza serikali ya mpito hadi baada ya siku 90 utakapoitishwa uchaguzi mkuu nchini humo.
Hata hivyo kwa vile hakuna mtu yeyote aliyejitokeza kugombea urais, uchaguzi huo umeakhirishwa, na utawala wa Bin Saleh nao umerefushwa.