Sisitizo la kutekelezwa makubaliano ya kugawana madaraka Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54623-sisitizo_la_kutekelezwa_makubaliano_ya_kugawana_madaraka_sudan
Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan ameahidi kwamba, baraza hilo litatekeleza kikamilifu makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Muungano wa Uhuru na Mageuzi na kwamba, linaunga mkono makubaliano hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2019 02:07 UTC
  • Sisitizo la kutekelezwa makubaliano ya kugawana madaraka Sudan

Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan ameahidi kwamba, baraza hilo litatekeleza kikamilifu makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Muungano wa Uhuru na Mageuzi na kwamba, linaunga mkono makubaliano hayo.

Abdul Fattah al Burhan ameyasema hayo baada ya baraza hilo kufikia makubaliano ya kugawana madaraka na kuunda serikali ya kiraia na vyama vya upinzani. Ameongeza kuwa nchi hiyo imeingia katika awamu mpya na kusisitiza udharura wa kuchungwa haki za kiraia na kupambana na ufisadi.

Abdul Fattah al Burhan, Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan
 

Majuzi wawakilishi wa Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan na muungano wa upinzani wa  Uhuru na Mabadiliko walifikia makubaliano ya kuunda serikali ya kiraia na baraza la utawala litakaloongoza serikali hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu. Pande hizo mbili pia zimekubaliana kufanya uchunguzi wa wazi na kamili kuhusu machafuko na ukatili uliofanyika nchini Sudan katika wiki kadhaa za hivi karibuni.

Baraza la Kijeshi la Sudan lilichukua madaraka tarehe 11 Aprili mwaka huu baada ya jeshi la nchi hiyo kumpindua Omar Hassan al-Bashir aliyekuwa rais wa nchi hiyo. Hata hivyo utendaji wa baraza hilo, kukataa kukabidhi madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia, uhusiano wa baadhi ya wanachama wake na nchi kama Saudi Arabia na Imarati, kuongezeka uingiliaji kati wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Sudan na vilevile misaada ya kifedha na kijeshi ya nchi hizo kwa Baraza la Kijeshi la Sudan na ukatili na mauaji yaliyofanywa na askari usalama dhidi ya waandamanji wasiopungua 120 yote hayo yamezidisha malalamiko na upinzani wa Wasudan dhidi ya watawala wa kijeshi wa nchi hiyo.

 Baada ya al Bashir kuondolewa madarakani kulifanyika vikao kadhaa vya mazungumzo ya kukomesha machafuko baina ya Baraza la Kijeshi la Mpito na muungano wa upinzani; lakini mauaji yaliyofanywa na jeshi la Sudan hapo tarehe 3 mwezi uliopita wa Juni mjini Khartoum yalipelekea kusimama mazungumzo hayo ambapo upinzani ulitangaza uasi wa kiraia kote nchini na kuapa kwamba, ungeendeleza maandamano hadi matakwa ya wananchi yatakapotekelezwa. Hali hiyo ilizidisha mgogoro wa ndani nchini humo. Wapinzani wanaotaka kukabidhiwa madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia na kuelekea kwenye mfumo wa kidemokrasia, walikabiliwa na ngumi ya chuma na ukatili mkubwa wa wanajeshi. Maandamano makubwa ya nchi nzima yaliyofanyika tarehe 30 Juni ili kuwashinikiza wanajeshi wakabidhi haraka madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia yalikuwa kilele cha uasi wa kisiasa na kijamii nchini Sudan. Katika mandamano hayo pia raia kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa.

Kutokana na hali hiyo wawakilishi wa Ethiopia na Umoja wa Afrika (AU) ambao ni wapatanishi katika mgogoro wa ndani nchini Sudan walizitaka pande mbili hasimu kujiepusha na hatua yoyote inayozidisha machafuko na kuketi tena kwenye meza ya mazungumzo. Hatimaye juhudi za wapatanishi hao zilizaa matunda na siku chache zilizopita pande hazimu zilifikia makubaliano ya kugawana madaraka na kuunda serikali ya mpito. Makubaliano hayo yamevipa vya siasa nchini Sudan matumaini ya kuanza awamu na kipindi kipya cha uhai wa kisiasa nchini humo. Hata hivyo bado kuna wasiwasi iwapo wanajeshi wanaotawala Sudan watatekeleza ahadi zao na kuheshimu mapatano hayo au la.  

Vyama vya siasa nchini Sudan vinataka kukabidhiwa madaraka kwa utawala wa kiraia utakaokuwa na waziri mkuu na bunge na kukomeshwa mfumo wa kidikteta. Vilevile vyama hivyo vimetoa wito wa kuheshimiwa haki zote za kiraia, kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa, kufanyika uchunguzi wa muaji ya raia ya tarehe 3 Juni na kupambana na ufisadi uliokita mizizi ndani ya asasi za serikali na jeshi.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameeleza kufurahishwa kwake na mapatano ya pande hasimu nchini Sudan na kuzitaka pande zote kutekeleza mapatano hayo yote haraka iwezekanavyo. Guterres pia ametoa wito wa kutatuliwa matatizo yote yaliyobakia kupitia njia ya mazungumzo. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres
 

Kwa vyovyote vile, makubaliano yaliyofikiwa nchini Sudan baina ya watawala wa kijeshi wa nchi hiyo na muungano wa upinzani wa Uhuru na Mabadiliko yanatambuliwa kuwa ni hatua muhimu sana inayotayarisha uwanja mzuri wa kuiondoa nchi hiyo katika mgogoro mkubwa na hatari ambao umetishia kuitumbukiza nchi katika vita vya ndani.