UN yatilia mkazo udharura wa kuanza tena mazungumzo ya amani Sudan
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuanza tena mazungumzo baina ya wapinzani na watawala wa kijeshi nchini Sudan.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya haki za binadamu, Andrew Gilmour amekiambia kikao cha Baraza la Haki za Binadamu cha umoja huo mjini Geneva kwamba: "Tunazihamasisha pande zote husika nchini Sudan kuendelea kutafuta utatuzi wa matatizo yaliyopo kupitia mazungumzo ambayo hayakukamilika."
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema umoja huo unapongeza na kukaribisha suala la kufanyika uchunguzi huru kuhusu ukatili na mauaji ya waandamanaji lililosisitizwa katika makubaliano ya amani yaliyofikiwa Alkhamisi iliyopita baina ya pande hizo mbili.
Andrew Gilmour amesema zimepatikana ripoti kamili na za kina kuhusu ukatili mkubwa uliofanyika tarehe 30 Juni katika miji mbalimbali ya Sudan na kuongeza kuwa: Jambo muhimu zaidi ni kuhakikisha kwamba, uchunguzi huo unawatendea haki na uadilifu wahanga wote wa ukatili huo na kutambua rasmi haki zao.
Gilmour amesema ana matarajio kwamba, makubaliano mapya baina pande mbili nchini Sudan yatatayarisha uwanja mzuri utakaoyawezesha makundi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kwenda Sudan katika wiki zijazo kwa ajili ya kufungua ofisi ya kudumisha mazungumzo ya amani.
Zaidi ya raia 120 waliuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika hujuma iliyofanywa na askari usalama wa Sudan dhidi ya waandamanaji wanaowataka wanajeshi wanaotawala nchi hiyo kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.