Njama za Imarati na Marekani za kuibambikizia kesi Ikhwanul Muslimin zafichuliwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54823-njama_za_imarati_na_marekani_za_kuibambikizia_kesi_ikhwanul_muslimin_zafichuliwa
Naibu Mkuu wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri amefichua kile kilichojadiliwa katika mazungumzo yake na maafisa kadhaa wa nchi za nje katika jela muda mfupi baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Julai 2013 nchini Misri.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 17, 2019 08:27 UTC
  • Njama za Imarati na Marekani za kuibambikizia kesi Ikhwanul Muslimin zafichuliwa

Naibu Mkuu wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri amefichua kile kilichojadiliwa katika mazungumzo yake na maafisa kadhaa wa nchi za nje katika jela muda mfupi baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Julai 2013 nchini Misri.

Matamshi hayo ya Khairat al Shater yameelezwa katika kikao cha kuhukumiwa upya viongozi kadhaa wa Ikhwanul Muslimin kwa tuhuma za kuifanyia ujasusi harakati ya Hamas. Hii ni mara ya kwanza kwa  Khairat al Shater kutoa matamshi hayo tangu alipotiwa mbaroni zaidi ya miaka sita iliyopita. Akiwa ndani ya mahakama Naibu huyo wa harakati ya Ikhwanul Muslimin amepinga tuhuma zilizotolewa dhidi yake na dhidi ya watuhumiwa wengine akiwemo Muhammad Morsi rais wa zamani wa Misri kwamba walikuwa wakiifanyika ujasusi Hamas. 

Al Shater amefichua pia mazungumzo yaliyofanywa baina yake na Abdallah bin Zaid Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati, William Burns Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani na Bernardino Leon Mjumbe wa Umoja wa Ulaya siku kadhaa baada ya yeye kutiwa mbaroni. Amesema kuwa watu hao walimtaka akiri kwamba alikuwa akifanya ujasusi ili wanachama wa Ikhwanul Muslimin waachiwe huru. 

Muhammad Morsi

Naibu Mkuu wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri amesisitiza kuwa iwapo mazungumzo yoyote yatahesabiwa kuwa ni ujasusi kwa nini basi mazungumzo hayo yalifanyika jela tena kwa ruhusa ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Misri? Khairat amehoji kwa nini uhasama wa kisiasa unabadilishwa na kuwa tuhuma na jinai dhidi ya Ikhwanul Muslimin?

Itakumbukwa kuwa maelfu ya viongozi na wanachama wa harakati ya Ikhwanul Muslimin wanashikiliwa katika jela za Misri.