Kikao cha hati ya pili ya Katiba ya Sudan chaakhirishwa
Muungano wa Uhuru na Mabadiliko wa Sudan umesema kuwa, kikao cha kujadili hati ya pili ya Katiba ya nchi hiyo kimeakhirishwa.
Muungano huo umesema hayo katika taarifa yake ya jana na kuongeza kuwa, kikao cha pande mbili baina ya wapinzani hao na baraza la kijeshi la Sudan kilichokuwa kifanyike leo Ijumaa kujadili hati ya pili ya Katiba mpya ya Sudan kimeakhirishwa.
Muungano huo umeongeza kuwa, hatua za awali za kuingizwa ndani ya muswada wa Katiba mpya, hati inayohusiana na amani, zimeshachukuliwa.
Hata hivyo Muungano huo Uhuru na Mabadiliko nchini Sudan haukusema kikao kilichoakhirishwa leo kitafanyika lini tena.
Katika upande mwingine, ujumbe mmoja wa muungano huo wa wapinzani wa Sudan unaendelea na mazungumzo na makundi yenye silaha katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kuhusiana na makubaliano jumla ya kisiasa nchini Sudan.
Baraza la Kijeshi la Sudan hivi karibuni limefikia makubaliano rasmi ya kisiasa na Muungano wa Uhuru na Mabadiliko wa nchi hiyo kuhusiana na kuundwa baraza la mpito la kuongoza nchi hiyo katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye mabadiliko ya kimsingi nchini Sudan.
Baraza hilo la kuongoza Sudan linaundwa na watu 11, watano ni wanajeshi na watano ni raia kutoka Muungano wa Uhuru na Mabadiliko huku mmoja akiwa ni raia asiyependelea upande wowote. Uongozi wa baraza hilo ni wa kupokezana.