Mazungumzo baina ya mahasimu wa Sudan yapiga hatua nzuri
Mazungumzo baina ya Muungano wa Uhuru na Mabadiliko na kundi la wanajeshi wanaotawala Sudan yameripotiwa kupiga hatua kubwa katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Mazungumzo hayo mapana zaidi kuhusu mustakbali wa Sudan baada ya Omar al Bashir yalianza Jumamosi iliyopo yakishirikisha wawaskilishi wa Muungano wa Uhuru na Mabadiliko, makundi yanayobeba silaha na wanajeshi wanaotawala Sudan. Ajenda kuu ya mazungumzo hayo ni suala la makundi yanayobeba silaha, mchakato wa mapatano, jinsi ya kuunda serikali ya kipindi cha mpito na uratibu juu ya mabadiliko ya kidemokrasia nchini Sudan.
Msemaji wa Muungano wa Uhuru na Mabadiliko, Usamah al Sayyid anasema kuwa, wawakilishi wa makundi hayo wamefikia mwafaka kuhusu vipengee vyote vya makubaliano ya amani isipokuwa masuala yanayohusiana na vipaumbele vya mabadiliko ya kidemokrasia na mchakato wa amani kote nchini Sudan.
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika zimekuwa zikitilia mkazo udharura wa kukabidhiwa madaraka ya nchi huko Sudan kwa utawala wa kiraia.
Baraza la Kijeshi la Sudan lilishika hatamu za uongozi nchini humo baada ya jeshi kufanya mapinduzi ya Aprili 11 mwaka huu na kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar Hassan al Bashir.