Sudan yasambaratisha jaribio la mapinduzi; yawatia mbaroni maafisa kadhaa wa jeshi
Jeshi la Sudan limesema kuwa limesambaratisha jaribio la mapinduzi na kuwatia nguvuni maafisa kadhaa wa ngazi ya juu jeshini kwa kuhusika na njama hiyo iliyokusudiwa kukirejesha uongozini chama cha Omar al Bashir, rais wa Sudan aliyeng'olewa madarakani.
Baraza la Uongozi wa Mpito la Jeshi la Sudan lilichukua uongozi wa nchi baada ya kumpindua al Bashir tarehe 11 Aprili mwaka huu kufuatia wiki kadhaa za maandamano dhidi yake.
Shirika la Habari la SUDAN, SUNA limeripoti kuwa baraza hilo la kijeshi hivi sasa linashughulia hatua za mwisho za kuhitimisha makubaliano ya kugawana madaraka na muungano wa vyama vya upinzani kwa muda wa miaka mitatu ya kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu.
Baraza la Kijeshi linaloongoza Sudan limesema kuwa jaribio hilo la mapinduzi lililozimwa lilikuwa na lengo la kusambaratisha mapinduzi na kukirejesha madarakani chama cha Kongresi ya Taifa na pia kuvuruga hali ya mambo huko Sudan kabla ya kupatikana suluhisho la la kisiasa kwa ajili ya kuunda serikali ya kiraia.
Taarifa ya jeshi hilo imeongeza kuwa jaribio hilo la mapinduzi limewahusisha Jenerali Hashim Abdul Muttalib Ahmed Mkuu wa Vikosi vya Majeshi ya Sudan, idadi kadhaa ya maafisa wa jeshi wa ngazi ya juu kutoka jeshi la ulinzi la nchi hiyo na Idara ya Itelijinsia na Usalama pamoja na viongozi wa chama cha Kongresi ya Taifa na chama cha Kiislamu. Jenerali Bakri Saleh ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu hadi miezi michache kabla ya kung'olewa madakani al Bashir; ni miongoni mwa watu waliotiwa mbaroni.