Waandamanaji watano wakiwemo wanafunzi wauawa nchini Sudan
Waandamanaji watano wakiwemo wanafunzi wanne wameuawa kwa kupigwa risasi katika maandamano ya jana nchini Sudan.
Mauaji hayo yametokea siku moja tu kabla ya kuanza tena kwa mazungumzo kati ya utawala wa kijeshi na viongozi wa maandamano ikiwa ni katika juhudi za kufikia makubaliano ya mwisho kuhusu uongozi wa mpito.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, mji wa Al-Obeid, makao makuu ya Jimbo la Kordofan Kaskazini jana ulishuhudia maandamano makubwa. Duru za hospitali zinasema kuwa, waandamanaji watano wamepigwa risasi katika maandamano hayo ya amani.
Wakati huo huo, mazungumzo ya kuyatafutia ufumbuzi masuala yaliyobakia kati ya viongozi wa waandamanaji na utawala wa kijeshi nchini Sudan yalitarajiwa kuanza leo.

Baraza la kijeshi na viongozi wa maandamano tayari wamesaini makubaliano ya kugawana madaraka ambayo yanalenga kuunda baraza tawala la pamoja la kijeshi na kiraia ambalo kisha litapisha utawala wa kiraia
Wanajeshi wa Sudan walichukua madaraka baada ya kupinduliwa Rais wa nchi hiyo Omar al Bashir Aprili 11 mwaka huu, hata hivyo wananchi wangali wanasisitiza kuhusu takwa lao la kuundwa serikali ya kiraia nchini humo.
Baraza la kijeshi la uongozi wa mpito la Sudan na Muungano wa upinzani wa Uhuru na Mabadiliko tarehe nne mwezi huu walifikia mapatano kuhusu uendeshaji wa kipindi cha mpito huko Sudan kwa upatanishi wa Umoja wa Ulaya na Ethiopia