Wasudan watolewa mwito wa kufanya "maandamano ya mamilioni" leo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55114-wasudan_watolewa_mwito_wa_kufanya_maandamano_ya_mamilioni_leo
Jumuiya ya ajira nchini Sudan imetoa mwito wa kufanyika "maandamano ya mamilioni" nchini kote hii leo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 31, 2019 22:28 UTC
  • Wasudan watolewa mwito wa kufanya

Jumuiya ya ajira nchini Sudan imetoa mwito wa kufanyika "maandamano ya mamilioni" nchini kote hii leo.

Taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo imetaka yafanyike maandamano ya mamilioni hii leo na kutekelezwa kisasi cha uadilifu kwa waliohusika na mauaji ya wanafunzi katika mji wa El-Obeid ulioko kwenye jimbo la Kordofan Kaskazini.

Taarifa ya jumuiya ya ajira nchini Sudan imeongeza kuwa, maandamano hayo ya leo yatafanyika katika mji mkuu Khartoum na miji mingine ya nchi hiyo kwa kaulimbu ya "Kuuliwa mwanafunzi mmoja ni sawa kuuliwa umma mzima".

Muungano wa upinzani wa "Uhuru na Mabadiliko" nao pia umesema, Baraza la Kijeshi ndilo linalobeba dhima ya matukio ya mji wa El-Obeid na kusisitizia ulazima wa kuadhibiwa waliohusika na jinai hiyo sambamba na kufanyika maandamano ya kulaani.

Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki, amesema, ameghadhibishwa na kuuawa waandamanaji katika mji wa El-Obeid na kutilia mkazo ulazima wa kulindwa haki ya kuandamana kwa amani na kudhaminiwa usalama wa raia wote hususan watoto.

Wanafunzi sita waliuliwa kwa kupigwa risasi siku ya Jumatatu wakati askari usalama wa Sudan walipokuwa wakiwatawanya wanafunzi hao walioandamana kulalamikia uhaba wa mafuta na mikate katika mji wa El-Obeid, mkoani Kordofan Kaskazini.../