Umoja wa Afrika wataka wauaji wa wanafunzi wa Sudan wafikishwe mahakamani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55116-umoja_wa_afrika_wataka_wauaji_wa_wanafunzi_wa_sudan_wafikishwe_mahakamani
Umoja wa Afrika (AU) umeitaka serikali ya Sudan kuwafikisha mahakamani askari waliohusika na mauaji ya wanafunzi 6 waliokuwa wakiandamana kulalamikia hali mbaya ya maisha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 01, 2019 02:54 UTC
  • Umoja wa Afrika wataka wauaji wa wanafunzi wa Sudan wafikishwe mahakamani

Umoja wa Afrika (AU) umeitaka serikali ya Sudan kuwafikisha mahakamani askari waliohusika na mauaji ya wanafunzi 6 waliokuwa wakiandamana kulalamikia hali mbaya ya maisha.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika katika masuala ya Sudan, Mohamed Hassan Labat ametoa wito wa kukamatwa na kufikishwa mahakamani watu waliohusika na mauaji ya wanafunzi hao. 

Labat pia ametoa wito wa kutayarishwa haraka rasimu ya katiba mpya ya Sudan na kusisitiza kuwa, ucheleweshaji wa aina yoyote wa kadhia hiyo utakuwa na madhara kwa nchi hiyo na bara zima la Afrika. 

Wakati huo huo Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki ameelezea kukasirishwa sana na mauaji ya waandamanaji yaliyofanywa na askari jeshi katika mji wa Al-Obeid, makao makuu ya Jimbo la Kordofan Kaskazini na amesisitiza udharura wa kulindwa haki ya kufanya maandamano na mikusanyiko ya amani na kulindwa usalama wa raia wote hususan watoto. 

Moussa Faki

Wanafunzi 6 walioshiriki katika maandamano hayo waliuawa siku ya Jumatatu katika ghasia zilizoibuka katika mji wa al Obeid kaskazini mwa mkoa wa Kordofan huko Sudan. Wanafunzi waliandamana kulalamikia uhaba wa mafuta na mkate.

Baraza la Kijeshi la Uongozi wa Mpito la Sudan lilichukua hatamu za uongozi baada ya jeshi kufanya mapinduzi na kumuondoa marakani Rais Omar al Bashir Aprili 11 mwaka huu. Hata hivyo wananchi wangali wanaandamana wakishinikiza kuundwa serikali ya kiraia huko Sudan.