Wasudan wafikia mapatano juu ya tangazo la katiba ya kipindi cha mpito
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55154-wasudan_wafikia_mapatano_juu_ya_tangazo_la_katiba_ya_kipindi_cha_mpito
Baraza la Kijeshi linalotawala Sudan na vyama vya upinzani wamefikia makubaliano juu ya tangazo la katiba ambayo itapelekea kuundwa serikali ya kipindi cha mpito nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 03, 2019 02:50 UTC
  • Wasudan wafikia mapatano juu ya tangazo la katiba ya kipindi cha mpito

Baraza la Kijeshi linalotawala Sudan na vyama vya upinzani wamefikia makubaliano juu ya tangazo la katiba ambayo itapelekea kuundwa serikali ya kipindi cha mpito nchini humo.

Mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa Sudan, Mohamed Hassan Labat amesema kuwa, wajumbe wa Baraza la Kijeshi na kambi ya upinzani ya Muungano wa Uhuru na Mabadiliko leo Jumamosi watakutana kujadili masuala ya kiufundi ya kupeleka mbele zaidi mwenendo wa kuunda serikali ya kipindi cha mpito. 

Labat ameongeza kuwa, katika utangulizi wa rasimu ya katiba hiyo, kikosi cha Radiamali ya Haraka cha Sudan kimeahidi kuwa chini ya Mkuu wa Majeshi ya Sudan katika kipindi cha utawala wa mpito.

Pande mbili zinazozozana nchini Sudan zimekubaliana kuunda serikali ya mpito itakayoongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 3. Serikali hiyo itakuwa na baraza la uongozi litakalokuwa na wanajeshi 5 na raia 5 na mkuu wake atateuliwa kwa zamu.

Wasudan wafikia makubaliano juu ya katiba ya kipindi cha mpito

Kwa sasa Sudan inatawali na kundi la wanajeshi lililotwaa madaraka baada ya kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar al Bashir Aprili 11 mwaka huu. 

Wananchi wa Sudan wamekuwa wakifanya maandamano wakitaka kukabidhiwa madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia. Vilevile wanataka wale wote waliohusika na mauaji ya waandamanaji wafikishwe mahakamani.