Maafikiano ya kuunda serikali ya mpito nchini Sudan
Baada ya kupita miezi kadhaa ya mzozo wa kisiasa nchini Sudan hatimaye Baraza la Kijeshi la Mpito na muungano mkuu wa wapinzani wa nchi hiyo wameafikiana juu ya tamko la katiba ambalo litapelekea kubuniwa serikali ya mpito nchini humo.
Kwa mujibu wa utangulizi wa tamko hilo la katiba, katika kipindi cha mpito, serikali ya kitaifa itaundwa ambapo itakuwa na jukumu la kuendesha mambo ya nchi na pia bunge jipya kubuniwa. Katika kipindi hicho cha mpito kikosi cha radiamali ya haraka kitawekwa chini ya kamandi kuu ya jeshi la Sudan. Kwa mujibu wa mapatano ya pande mbili, kipindi cha mpito kitakuwa cha miaka mitatu na miezi mitatu ambapo Baraza la Utawala litakuwa na wanachama 6 wa kiraia na 5 wa kijeshi ambao watakuwa wakiliongoza kwa zamu.
Akifafanua suala hilo, Mohamed Hassan Lebatt, mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa Sudan amesema: Baraza la Kijeshi linalotawala Sudan na viongozi wa wafanyamaandamano wameafikiana juu ya tamko la katiba ambalo linafungua njia ya kukabidhiwa madaraka kwa raia.
Hata kama kupinduliwa Rais Omar al-Bashir wa Sudan tarehe 11 Aprili mwaka huu kulihesabiwa kuwa hatua muhimu katika mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo lakini kubuniwa Baraza la Kijeshi na utendaji wake katika miezi minne iliyopita umepelekea kuongezeka malalamiko na maandamano ya wananchi na hivyo kuharibu zaidi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo. Kutotaka baraza hilo kukabidhi madaraka kwa raia, kuuliwa waandamanaji na uhusiano wa baraza hilo la Saudi Arabia, Imarati na Misri ambao umezidisha uingiliaji wa wageni katika mambo ya ndani ya Sudan ni masuala ambayo yamewakasirisha sana wananchi wa nchi hiyo.
Tangu Baraza la Kijeshi la Mpito libuniwe, si tu kwamba baraza hilo halijakuwa na nia ya kuwashirikisha raia katika uendeshaji wa mambo ya Sudan bali limekuwa likisitasita kubuni serikali ya mpito itakayoandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru na wa kidemokrasia nchini. Katika upande wa pili, kuuawa makumi ya Wasudan walioshiriki maandamano ya amani dhidi ya baraza hilo kumevikasirisha sana vyama vya siasa vya nchi hiyo. Kukabidhiwa raia madaraka na kuandaliwa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru kwa ajili ya kubuniwa serikali ya kidemokrasia ni matakwa muhimu ya wapinzani na vyama vya siasa vya Sudan. Kuheshimiwa haki za kiraia, kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa, kubuniwa tume ya uchunguzi kwa ajili ya kufuatilia mauaji ya tarehe 3 Juni na kupambana na ubadhirifu wa mali ya umma ni miongoni mwa matakwa ya vyama vya siasa.
Uingiliaji wa kigeni katika mambo ya ndani ya Sudan pia umeongezeka sana katika miezi kadhaa iliyopita. Saudia, Imarati na Misri ni miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa Baraza la Kijeshi la Sudan ambao wanafanya juhudi za kudhamini maslahi yao nchini humo kupitia baraza hilo. Kulinda ushiriki wa askari wa Sudan katika muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen ni moja ya malengo muhimu ya kutolewa uungaji mkono wa nchi tatu hizo kwa Baraza la Kijeshi la Sudan. Hii ni katika hali ambayo makundi ya upinzani ya Sudan yanataka kukatwa kwa kila aina ya uingiliaji wa kigeni katika mambo ya ndani ya nchi hiyo.
Hata kama kubuniwa kwa serikali ya mpito linaweza kuwa suluhisho la mgogoro wa Sudanb lakini bado kuna mambo mengi yasiyoeleweka wala kubainishwa vyema kuhusiana na jinsi ya kutekelezwa mapatano yaliyofikiwa kati ya pande mbili. Miongoni mwa mambo yenye utata ni pamoja na uwezo wa Baraza la Utawala, kutumwa askari usalama sehemu za ghasia na kinga ya kisheria ya majenerali waliohusika katika ukandamizaji wa waandamanaji na hasa wale waliohusika na mauaji ya Wasudan waliokuwa wamekusanyika mjini Khartoum tarehe 3 Juni.
Abdul Hamid Awadh, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na suala hilo: Kutoaminiana pande mbili, uwezekano wa kufanyika mapinduzi ya kijeshi, uingiliaji wa nchi za eneo na matatizo ya kiuchumi ni miongoni mwa mambo yanayohatarisha utekelezaji wa mapatano yaliyofikiwa hivi karibuni.
Hata kama bado kuna matatizo mengi katika njia ya utekelezaji wa maafikiano hayo lakini ni wazi kuwa sasa Baraza la Kijeshi la Sudan na wapinzani wanachukulia utekelezaji wa maafikiano hayo kuwa lengo lao la pamoja. Wanatambua vyema kwamba njia pekee ya kuiondolea Sudan mgogoro wa hivi sasa, ni kutembea kwenye njia ya demokrasia na kupunguza uingiliaji wa kigeni.