Wanajeshi na wapinzani Sudan watiliana saini tamko la kuunda serikali ya mpito
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55198-wanajeshi_na_wapinzani_sudan_watiliana_saini_tamko_la_kuunda_serikali_ya_mpito
Hatimaye baada ya vuta nikuvute wanajeshi na viongozi wa waandamanaji nchini Sudan wametiliana saini tamko la katiba litakalowaongoza katika kuunda serikali ya mpito.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 05, 2019 03:52 UTC
  • Wanajeshi na wapinzani Sudan watiliana saini tamko la kuunda serikali ya mpito

Hatimaye baada ya vuta nikuvute wanajeshi na viongozi wa waandamanaji nchini Sudan wametiliana saini tamko la katiba litakalowaongoza katika kuunda serikali ya mpito.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, kiongozi wa waandamanaji Ahmed Rabie na naibu kiongozi wa baraza la kijeshi Jenerali Mohamed Hamdan Daglo, ndio waliotia saini mkataba huo ulioshuhudiwa na wasuluhishi kutoka nchini Ethiopia na Umoja wa Afrika.

Kwa mujibu wa mkataba huo, katika kipindi cha mpito, serikali ya kitaifa itaundwa ambapo itakuwa na jukumu la kuendesha mambo ya nchi na pia bunge jipya kubuniwa. Katika kipindi hicho cha mpito kikosi cha radiamali ya haraka kitawekwa chini ya kamandi kuu ya jeshi la Sudan.

Kwa mujibu wa mapatano ya pande mbili, kipindi cha mpito kitakuwa cha miaka mitatu na miezi mitatu ambapo Baraza la Utawala litakuwa na wanachama 6 wa kiraia na 5 wa kijeshi ambao watakuwa wakiliongoza kwa zamu.

Kadhalika imekubaliwa kuwa, kamati maalumu iundwe ili kuchunguza mauaji ya mamia ya watu waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya kushinikiza kuachia madaraka rais wa zamani Omar al-Bashir.

Sudan ilianza kushuhudia wimbi la maandamano ya wananchi kuanzia katikati ya mwezi Disemba mwaka jana dhidi ya hali mbaya ya uchumi; na kufuatia ghasia hizo jeshi la Sudan tarehe 11 Aprili mwaka huu lilimpindua madarakani rais huyo wa zamani na kushika hatamu za uongozi kwa kuunda  baraza la kijeshi.