Njama ya mapinduzi ya jamaa wa al Bashir yagunduliwa Sudan
Gazeti moja la Sudan limeripoti kuwa, watu wenye mfungamano na rais aliyeondolewa madarakani nchini huko wanatayarisha mpango wa kufanya mapinduzi katika sikukuu ya Idul Adh'ha.
Gazeti la la Intibaha limeripoti kuwa, wapinzani wa Sudan wamegundua njama inayofanywa na kundi la maafisa wa zamani wa serikali iliyoondolewa madarakani ya Omar al Bashir ya kutekeleza mauaji na kuzusha hali ya hofu ya machafuko nchini humo katika sikukuu ya Idul Adh'ha kwa shabaha ya kufanya mapinduzi.
Ripoti ya gazeti hilo imesema kuwa, wafuasi wa Omar al Bashir wamepanga njama ya kuzusha ghasia na machafuko, kufanya mauaji katika siku ya Idi na kutekeleza mapinduzi dhidi ya serikali ya sasa ambayo tayari imechukua hatua za dharura za kukabiliana na njama hiyo.
Tangu serikali ya Omar al Bashir ilipoondolewa madarakani tarehe 11 Aprili mwaka huu, Baraza la Kijeshi linaloongoza nchi hiyo limedai mara kadhaa kwamba, limezima majaribio ya mapinduzi nchini Sudan.
Tarehe 12 Julai baraza hilo lilidai kuwa limezima jaribio la mapinduzi na kuwatia nguvuni maafisa 16 wa jeshi kuhusiana na jaribio hilo. Vilevile tarehe 24 mwezi huo huo watawala wa sasa wa Sudan walisema kuwa, wamewakamata maafisa kadhaa wa zamani wa jeshi kwa kuhusika na njama ya mapinduzi.