Kutiwa saini hati ya katiba nchini Sudan na mustakbali wa nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55456-kutiwa_saini_hati_ya_katiba_nchini_sudan_na_mustakbali_wa_nchi_hiyo
Hatimaye baada ya kupita miezi minne tangu kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan yaliyomuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir na kisha kuundwa Baraza la Kijeshi la Mpito, kumetiwa saini hati ya mwisho ya katiba ambayo inafungua uwanja wa kukabidhiwa madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 18, 2019 07:38 UTC
  • Kutiwa saini hati ya katiba nchini Sudan na mustakbali wa nchi hiyo

Hatimaye baada ya kupita miezi minne tangu kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan yaliyomuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir na kisha kuundwa Baraza la Kijeshi la Mpito, kumetiwa saini hati ya mwisho ya katiba ambayo inafungua uwanja wa kukabidhiwa madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.

Hati hiyo ya mwisho ya tangazo la katiba ilitiwa saini jana Jumamosi mjini Khartoum baina baina ya kiongozi wa waandamanaji Ahmed Rabie na kiongozi wa baraza la kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan. Aidha wawakilishi kutoka nchi mbalimbali walishiriki katika hafla hiyo ya utilianaji saini ambao unahesabiwa kuwa muhimu kwa Sudan baada ya miezi kadhaa ya vuta nikuvute na maandamano yya wananchi. Kwa muktadha huo, kipindi cha utawala wa mpito wa miaka mitatu kimeanza rasmi nchini Sudan.

Hati hiyo ya makubaliano ya kuunda serikali ya mpito imetiwa saini katika hali ambayo, Sudan ilianza kushuhudia mgogoro wa kisiasa tangu Disemba mwaka jana.

Awali maandamano ya wananchi nchini Sudan yalikuwa yakilalamikia hali mbaya ya kiuchumi na sera za Rais Omar al-Bashir. Hata hivyo baadaye maandamano hayo yalichukua mkondo wa kisiasa baada ya vyama muhimu kujiunga na maandamano hayo ya wananchi. Kufuatia hali hiyo, matakwa ya wananchi hao nayo yakachukua wigo mpana zaidi.

 

Wananchi wa Sudan wakisherehekea  kutiwa saini makubaliano ya kuundwa serikali ya mpito

Kufuatia kushadidi ghasia na maandamano, jeshi la Sudan tarehe 11 Aprili mwaka huu lilimpindua madarakani Omar al-Bashir na kuchukua hatamu za uongozi kwa kuunda  baraza la kijeshi ambalo lilitangaza kuwa, litaongoza nchi hiyo kwa muda wa miaka mitatu. Hata hivyo, utendaji na harakati za majenerali wa jeshi waliochukua madaraka ya nchi zikaswa kinyume na malengo ya waandamanaji. Waandamanaji walikuwa wakitaka kuhitimishwa utawala wa kijeshi na kupatikana uhuru wa kisiasa kupitia kuundwa serikali ya kidemokrasia kwa mujibu wa kura za wananchi na kuhitimishwa uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo, msimamo ambao haukuheshimiwa wala kuzingatiwa na Baraza la Kijeshi la Mpito.

Mauaji ya Juni 3 mwaka huu na kuweko uhusiano mkubwa baina ya Baraza la Kkijeshi la Mpito la Sudan na Saudi Arabia na Imarati ikawa nukta ya kudhihiri siku baada ya siku ghadhabu za wananchi na hivyo kupanuka wigo wa maandamano na malalamiko yao dhidi ya majerali hao wa jeshi. Mazingira hayo yalipelekea kuanzishwa mazungumzo ya kuhitimisha mgogoro wa Sudan na pande mbili zikaafikiana juu ya kutiliana saini hati ya katiba.

Filihali wapinzani  na Baraza la Kijeshi la Mpito wametiliana saini hati ambayo imeleta matumaini makubwa kwa akthari ya wananchi wa Sudan, kwani kupitia hati hiyo, kutarahisishwa mchakato wa kupatikana serikali ya kidemokrasia kwa mujibu wa kura za wananchi wa nchi hiyo. 

Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Kiijeshi la Mpito

Kwa mujibu wa mapatano ya pande mbili, kipindi cha mpito kitakuwa cha miaka mitatu na miezi mitatu ambapo Baraza la Utawala litakuwa na wanachama 6 wa kiraia na 5 wa kijeshi ambao watakuwa wakiliongoza kwa zamu. 

Aidha kwa mujibu wa mkataba huo, katika kipindi cha mpito, serikali ya kitaifa itaundwa ambapo itakuwa na jukumu la kuendesha mambo ya nchi na pia bunge jipya kubuniwa. Kadhalika katika kipindi hicho cha mpito, kikosi cha radiamali ya haraka kitawekwa chini ya kamandi kuu ya jeshi la Sudan. Vilevile imekubaliwa kuwa, kamati maalumu iundwe ili kuchunguza mauaji ya mamia ya watu waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya kushinikiza kuachia madaraka rais wa zamani Omar al-Bashir.

Akizungumza katika hafla ya utilianaji saini huo, Jenerali Abdul-Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Kiijeshi la Mpito alisema: Mapinduzi ya Sudan yamefikia malengo yake kwa juhudi za wananchi na kuwa kwake ni ya amani ni jambo litakalobakia katika kumbukumbu za walimwengu.

Katika uwanja huo, tayari kumeanza mazungumzo ya kumteua Waziri Mkuu. Muungano wa upinzani wa Uhuru na Mabadiliko nchini Sudan umeafiki kuteuliwa kwa Abdullah Hamdok kuwa Waziri Mkuu wa serikali ya mpito na kuahidi kumuunga mkono. Dkt Hamdok aliyependekezwa kuwa Waziri Mkuu ni mtaalamu wa masuala ya kifedha na uchumi na amewahi kufanya kazi na mashirika ya kimataifa na pia Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi wa Afrika (UNECA).

Abdullah Hamdok aliyependekezwa kushika wadhifa wa Waziri Mkuu

Kuleta mabadiliko ya muundo, kuboresha hali ya uchumi, kufuatilia faili la mauaji ya Junii 3, kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa na kurejesha amani na usalama nchini Sudan ni miongoni mwa matakwa muhimu ya makundi ya upinzani nchini humo.

Licha ya kuwa baada ya kutiwa saini hati ya katiba ya muda kumeleta matumiani kwa akthari ya wananchi wa Sudan kwamba, nchi yao imepiga hatua kuelekea upande wa demokrasia, lakini akthari yao pia wana wasiwasi wa ushawishi na kuendelea kuweko nguvu ya wanajeshi sambamba na uingiliaji wa kigeni katika mustakbali wa kisiasa wa nchi hiyo.