Sudan yaakhirisha kuvunja Baraza la Kijeshi la Mpito
Hatua ya kulivunja Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan ambayo ilikuwa itekelezwe leo, imeakhirishwa kwa muda wa masaa 48 yajayo.
Shams al-Din Kabashi, msemaji wa Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan ametangaza leo kuwa, uvunjwaji wa baraza hilo umesogezwa mbele kwa masaa 48 ili kutoa fursa ya kutangazwa majina ya watu watakaoongoza Baraza la Utawala wa Mpito kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande mbili kupitia tangazo la katiba.
Kwa mujibu wa hati ya mwisho ya katiba iliyotiwa saini Jumamosi iliyopita, Baraza la Kijeshi la Mpito linapaswa kuvunjwa na nafasi yake kuchukuliwa na Baraza la Utawala wa Mpito litakaloongoza Sudan kuelekea uchaguzi mkuu.
Muungano wa Uhuru na Mabadiliko unaowakilisha mirengo na makundi ya waandamanaji nchini Sudan umetangaza majina ya wawakilishi wake wanne katika Baraza la Utawala la nchi hiyo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, vikao vya mashauriano vingali vinaendelea kwa ajili ya kumteua mjumbe wa tano wa mrengo huo wa kiraia katika Baraza la Utawala la Sudan litakalojumuisha pia jeshi la nchi hiyo.
Viongozi wa upinzani na wa Baraza la Kijeshi siku ya Jumamosi walisaini hati ya mwisho ya katiba, ambayo inafungua uwanja wa kukabidhiwa madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na wa nchi za eneo pamoja na wawakilishi wa taasisi za kimataifa.