Hatimaye Baraza la Utawala wa Mpito laundwa nchini Sudan
Hatimaye Baraza la Utawala wa Mpito nchini Sudan limeundwa baada ya miezi kadhaa ya maandamano na mivutano tangu alipoondolewa madarakani Omar Hassan al-Bashir.
Baraza la Utawala wa Mpito nchini Sudan litaongozwa na wajumbe 11 wakiwemo sita wa kiraia na wanajeshi watano na litaongoza kwa muda wa miaka 3 kuelekea uchaguzi mkuu.
Kwa kuanzia baraza hilo litaongozwa na Abdul-Fattah al-Burhan aliyekuwa Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito ambalo sasa limevunjwa na nafasi yake kuchukuliwa na Baraza la Utawala.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, wajumbe watano wa kijeshi katika baraza jipya la utawala wa mpito ni majenerali Abdul-Fattah al-Burhan, Mohammed Hamdan Dagalo, Yasser Atta, Ibrahim Gaber na Shams al-Din Kabashi.
Aidha wajumbe wa muungano wa upinzani katika baraza hilo la utawala ni Hassan Mohamed Idris, Al-Siddiq Tawer Kafi, Ayesha Musa Saeed, Mohamed Osman Hassan al-Taayeshi na Raja Nicola Issa Abdul-Masseh. Katika orodha hiyo ya muuungano wa upionzani yumo mwanamke mmoja na mwandishi wa habari.
Aidha Abdalla Hamdok ambaye kitaaluma ni mchumi anatarajiwa kuapishwa leo kuchukua nafasi ya Wazirii Mkuu.
Kwa mujibu wa mapatano ya pande mbili, Baraza la Utawala wa Mpito litakaloongoza kwa muda wa miaka mitatu litakuwa na wanachama 6 wa kiraia na 5 wa kijeshi ambao watakuwa wakiliongoza kwa zamu.