Serikali mpya ya Sudan yaomba kusaidiwa kifedha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55588-serikali_mpya_ya_sudan_yaomba_kusaidiwa_kifedha
Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan amesema kuwa, nchi hiyo inahitajia msaada wa kigeni wa dola bilioni nane kwa ajili ya kufufua uchumi wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 25, 2019 03:26 UTC
  • Serikali mpya ya Sudan yaomba kusaidiwa kifedha

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan amesema kuwa, nchi hiyo inahitajia msaada wa kigeni wa dola bilioni nane kwa ajili ya kufufua uchumi wake.

Abdalla Hamdok alisema hayo jana katika mahojiano na shirika la habari la Reuters na kuongeza kuwa, katika kipindi cha miaka miwili ijayo, Sudan italazimika kulipa madeni na kufanya juhudi kubwa za kufufua uchumi wake kwani imedhoofishwa sana na mgogoro wa miezi kadhaa sasa wa kisiasa. Amesema, Sudan hivi sasa inahitaji msaada wa kigeni wa dola bilioni nane kuweza kukabiliana na changamoto zake nyingi hasa za kiuchumi.

Ameongeza kuwa, mazungumzo baina yake na Mfuko wa Kimataifa wa Fedha na Benki ya Dunia yameshaanza kama juhudi za kuyashawishi mashirika hayo muhimu ya kifedha ya kimataifa kuipatia tena mikopo Sudan.

Majenerali wa kijeshi waliohodhi madaraka nchini Sudan

 

Jumatano iliyopita, Abdalla Hamdok alikula kiapo cha kuwa Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Sudan.

Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan limekuwa likitawala nchini humo tangu tarehe 11 Aprili baada ya kupinduliwa Jenerali Omar al Bashir. Mara kwa mara baraza hilo la mpito lilikuwa likituhumiwa kukwamisha mambo ili kuzuia utawala wa raia nchini humo, lakini kusimama imara wananchi katika maandamano kumelilazimisha baraza hilo la kijeshi linaloungwa mkono na Saudi Arabia, Imarati na Misri lisalimu amri na kuruhusu kushirikishwa kikamilifu wananchi katika utawala.