Watu 37 wauawa katika mapigano ya kikabila nchini Sudan
Vyombo vya habari vya Sudan vimeripoti kuwa watu wasiopungua 37 wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyotokea mashariki mwa nchi hiyo.
Gazeti la Sudan Tribune limeripoti leo kuwa, mbali na watu 37 waliouawa, 200 wengine wamejeruhiwa katika mapigano kati ya makabila ya Bani Amer na Nuba mashariki mwa nchi hiyo. Hata hivyo chanzo hasa cha mapigano hayo bado hakijajulikana.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, majeruhi wa mapigano hayo wamekimbizwa hospitalini.
Katika radiamali na hatua liliyochukua kuhusiana na mapigano hayo ya kikabila, siku ya Jumapili, Baraza la Utawala la Sudan lilitangaza hali ya hatari katika jimbo la Bahari Nyekundu na kumwachisha kazi Gavana na Naibu Mkuu wa vyombo vya usalama katika jimbo hilo kwa kuzembea kuchukua hatua za kuzuia kutokea mapigano hayo.
Baraza hilo aidha limeamuru ufanyike uchunguzi kuhusu mapigano hayo na kusisitiza kuwa litawachukulia hatua waliosababisha kutokea kwake.
Mapigano hayo ya kikabila kati ya kabila la Bani Amer na lile la Nuba yalianza siku ya Alkhamisi iliyopita katika bandari ya Sudan makao makuu ya jimbo la Bahari Nyekundu.../